Mar 13, 2022 03:25 UTC
  • Watu 60 waaga dunia katika ajali ya treni Kongo DR

Kwa akali watu 60 wamepoteza maisha katika ajali mbaya ya treni iliyotokea katika mkoa wa Lualaba, kusini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Treni hiyo ilikuwa ikitokea mji wa Mueneditu ikielekea Lubumbashi.

Jean-Serge Lumu, afisa wa serikali katika mkoa huo alitangaza habari hiyo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, garimoshi hilo la kusafirishia mizigo liliacha reli Ijumaa jioni na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 60 huku wengine wengi wakijeruhiwa.

Amesema akthari ya majeruhi akiwemo mtoto mwenye umri wa chini ya miaka miwili ambaye wazazi wake wameaga dunia kwenye ajali hiyo, wamelazwa katika hospitali moja iliyoko katika eneo la Lubudi mkoani Lualaba.

Duru za habari zinaarifu kuwa, idadi hiyo iliyotolewa na serikali ni ya muda, na yumkini ikaongezeka kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata abiria. 

Ramani ya DRC

Ajali kubwa za treni zimekuwa zikitokea mara kwa mara huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni kuchakaa kwa reli, magarimoshi na mabehewa ambayo ni ya tangu enzi za ukoloni katika muongo wa 60.

Mwezi Machi mwaka 2019, ajali nyingine ya garimoshi la kusafirishia mizigo ilitokea katika mkoa wa Kasai wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kupelekea watu 50 kupoteza maisha huku wengine wapatao 80 wakijeruhiwa.

Tags