Apr 01, 2022 10:25 UTC
  • Mapigano ya kikabila Darfur yasababisha vifo vya makumi ya watu

Mapigano makali kati ya makundi hasimu huko Darfur nchini Sudan yamesababisha takriban watu 45 kuuawa, huku viongozi wa kikabila wakiripoti kwamba mapigano hayo ni sehemu ya ghasia za kikabila zinazoendelea katika eneo hilo.

Mapigano mapya yalizuka Jumanne wiki hii kati ya watu wa kabila la Kiafrika la Fallata na kabila moja la Kiarabu katika vijiji vya nje ya Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.

Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Usalama ya jimbo la Darfur Kusini imesema:  "Watu 15 waliuawa katika mapigano kati ya makabila ya Fallata na Rizeigat siku ya Jumanne, na 30 waliuawa siku ya Jumatano."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wanawake na watoto walikuwa miongoni mwa waliouawa katika mapigano hayo.

Duru za matibabu pia zimesema kuwa karibu watu 20 waliojeruhiwa, wengine vibaya, wamepelekwa katika hospitali za karibu na eneo hilo.

Jimbo lenye machafuko la Magharibi mwa Sudan la Darfur limeathiriwa na vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka 2003. 

Mzozo huo uliwakutanisha pamoja waasi wa makabila madogo madogo waliolalamikia kubaguliwa na serikali ya rais wa wakati huo wa Sudan, Omar al-Bashir iliyodhibitiwa na watu wa makabil ya Waarabu.

Darfur

Khartoum ilikabiliana na uasi hou kwa kutumia wapiganji wa kundi la Janjaweed, hasa walioajiriwa kutoka makabila ya wafugaji wa Kiarabu, ambao walilaumiwa kwa kufanya ukatili ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji, uporaji na kuchoma vijiji.

Umoja wa Mataifa unasema watu wasiopungua 300,000 wameuwa na wengine milioni 2.5 wamelazimika kukimbia makazi yao, kutokana na machafuko ya Darfur.

Tags