Jun 03, 2016 03:53 UTC
  • Watu karibu laki sita wanakabiliwa na baa la njaa Angola

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa watu laki tano na elfu 80 wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na baa la njaa nchini Angola.

Pier Paolo Balladelli, Mjumbe wa UN nchini Angola amesema watoto laki moja na elfu ishirini ni miongoni mwa watu hao wanaokabiliwa na baa la njaa. Taarifa ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, watu elfu arubaini wanakabiliwa na utapiamlo aghalabu yao wakitokea miji ya Namibe, Huíla, Cunene na Cuando Cubango ya kusini mwa nchi.

Umoja wa Mataifa ulisema katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba, kutokana na taathira za hali mbaya ya hewa maarufu kwa jina la Elnino mwaka huu, watu milioni 60 wataongezeka katika idadi ya watu wanaotaabika kwa njaa duniani ambapo nusu ya idadi hiyo wanapatikana barani Afrika.

Hivi karibuni Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ulitangaza kuwa, watoto milioni 11 wapo katika hatari ya kupoteza maisha katika nchi za mashariki na kusini mwa Afrika kutokana na athari za ukame.

Tags