Umoja wa Afrika wataka Russia iondolewe vikwazo
Vikwazo dhidi ya Russia katika nyanja ya usambazaji wa kimataifa wa nafaka na mbolea vinapaswa kuondolewa, Rais wa Senegal na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Macky Sall alisema Ijumaa baada ya mazungumzo na Rais wa Russia Vladimir Putin.
Akizungumza wakati alipokutana na Putin mjini Sochi, Russia, Rais Sall amesema, "Vikwazo dhidi ya Russia vilizidisha hali kuwa mbaya zaidi kutokana na kusitishwa usambazaji wa nafaka na mbolea kwa nchi za Afrika."
Amsema hivi sasa bara la Afrika halina bidhaa hizo muhimu ambazo zilikuwa zinanunuliwa Russia na Ukraine jambo ambalo limekuwa na matokeo mabaya kwa usalama wa chakula barani Afrika.
Sall amesema Senegal "inaunga mkono kutolewa kwa nafaka na mbolea kutoka kwa vikwazo dhidi ya Russia. Nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zimeiwekea Russia vikwazo vya kidhalimu kutokana na oparesheni zake za kijeshi nchini Ukraine. Vikwazo hivyo vimepelekea Russia isiweze kuuza nafaka hasa ngano na pia mbolea katika nchi za Afrika zinazohitajia bidhaa hizo muhimu.

Macky Sall alisisitiza jukumu muhimu la Russia katika historia ya bara la Afrika na kuelezea matumaini ya upanuzi wa ushirikiano.
Baada ya mazungumzo hayo yaliyodumu masaa matatu, Putin amewaambia waandishi wa habari kwamba Russia wakati wote iko upande wa Afrika na sasa inaangazia zaidi kuimarisha zaidi mahusiano.