Jun 05, 2016 04:12 UTC
  • Nigeria: Tumedhibiti mabilioni ya Dola zilizokuwa zimeporwa na mafisadi

Serikali ya Nigeria imetangaza kunasa na kudhibiti mali na fedha za umma zinazokaribia Dola bilioni 11 za Marekani zilizokuwa zimeporwa na mafisadi.

Hayo yalisemwa jana Jumamosi na Lai Mohammed, Waziri wa habari na Utamaduni wa Nigeria na kuongeza kuwa, katika harakati za kupambana na ufisadi wa fedha zilizoanza mwaka mmoja uliopita, hadi sasa serikali ya Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo imefanikiwa kudhibiti zaidi ya Dola bilioni 10 na milioni 300 za Marekani. Kwa mujibu wa Mohammed, kiasi hicho cha fedha kinatokana na mali mbalimbali na fedha tasilimu. Aidha Waziri huyo wa habari na Utamaduni amesema kuwa, Abuja inatarajia kuona kiasi cha Dola milioni 330 zilizochotwa kutoka hazina ya serikali na kuwekekwa katika benki za nje ya nchi hususan nchini Uswisi, zinarejeshwa katika hazina ya taifa. Amezitaja fedha na mali hizo zilizokamatwa kuwa ni pamoja na Dola milioni 583 na laki tano, Dola bilioni tisa na milioni 700 ambazo zinatokana na fedha tasilimu na mali nyingine kama vile meli, majengo na ardhi. Aidha katika harakati hizo za kupambana na ufisadi nchini Nigeria, mamia ya watu wametiwa mbaroni na kupandishwa kizimbani kati yao akiwa ni mshauri wa zamani wa usalama wa taifa ambaye anatuhumiwa kwa kupora kiasi cha Dola bilioni mbili na milioni 100.

Tags