Juhudi za Marekani za kueneza ushawishi wake barani Afrika
Akiwa katika safari yake ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika, Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, amezungumza na kushauriana na viongozi wa nchi alizozitembelea kuhusu masuala ya usalama, mgogoro wa chakula na jinsi ya kuzishirikisha nchi za Kiafrika katika vita vya Ukraine.
Katika safari hiyo, ametembelea Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda.
Hiyo ni ziara ya pili ya Anthony Blinken katika bara la Afrika tangu achukue nafasi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani.
Hivi sasa ambapo vita vya Ukraine vinaendelea, Marekani inajaribu kuzishawishi nchi mbalimbali kuchukua msimamo dhidi ya Moscow. Tangu kuanza vita vya Russia na Ukraine, nchi nyingi za Kiafrika zimetangaza wazi kuwa hazitafuata siasa za Washington kuhusu suala hilo na kwamba zitaendeleza uhusiano na Russia.
Katika miongo ya karibuni, nchi nyingi za Kiafrika zimezingatia uimarishaji wa sera za kikanda ili kudumisha uhuru na usalama wao, na zimekataa kufuata sera za Marekani na Ulaya katika uwanja huo. Kuhusu vita vya Russia na Ukraine, nchi nyingi za Kiafrika zimetangaza kwamba zitaendeleza uhusiano wao na Moscow na kuwa hazitafuata sera za Magharibi kuhusu jambo hilo.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini huku akisisitiza kuwa sera ya nchi hiyo ni kufikiwa suluhu ya kidiplomasia na ya kudumu kuhusu mzozo wa Ukraine, amesema: Kama NATO ingezingatia maonyo ya viongozi ambao wamekuwa wakisema kwa miaka mingi kuwa upanuzi wa shirika hilo la kijeshi kuelekea Ulaya Mashariki utavuruga zaidi usalama wa eneo hilo, vita kati ya Russia na Ukraine havingetokea.
Nchi za Kiafrika ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikikabiliwa na hali ya ukosefu wa usalama unaosababishwa na kuwepo kwa makundi ya kigaidi na uhaba wa chakula, sasa zina wasiwasi kuhusu ongezeko la matatizo ya chakula hususan ukosefu wa nafaka na chakula kutokana na athari za vita vya Ukraine. Mataifa ya Afrika sio tu yangali yanakumbuka vizuri miaka ya ukoloni, bali katika miaka miwili iliyopita na kufuatia kuenea maradhi ya Covid-19, yameshuhudia tena ukosefu wa ushirikiano wa Marekani na nchi za Magharibi kuhusu suala zima la kutoa dawa, chanjo na vifaa vya matibabu. Kwa kadiri kwamba katika nchi nyingi za bara hilo, ni chini ya asilimia moja ya watu ndio wamefanikiwa kupata chanjo ya corona.
Hali hiyo imewapelekea viongozi wengi wa Afrika kujikita zaidi katika kupanua mahusiano kwa kuzingatia mahitaji na sera za ndani za bara hilo. Kuhusiana na hilo, Rais Macky Sall wa Senegal ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, hivi karibuni alisafiri kwenda Russia ili kuifikishia kilio cha wasiwasi wa watu wa bara hilo, ambao wanakabiliwa na matatizo ya uhaba wa chakula.
Uhusiano na misimamo hiyo ya viongozi wa Afrika imewakasirisha viongozi wa Washington, na hasa ikitiliwa maanani kwamba hivi karibuni Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alizitembelea nchi kadhaa za Afrika. Mwishoni mwa safari yake hiyo, Lavrov alizikosoa nchi za Magharibi na kupinga madai kwamba mashambulizi ya Russia dhidi ya Ukraine ndiyo yamesababisha bei ya vyakula duniani kupanda. Amesisitiza kuwa bei tayari zilikuwa zinaongezeka kabla ya shambulio la Russia huko Ukraine, kwa sababu ya janga la Covid-19 na kile alichokiita kuwa 'sera za kijani' za nchi za Magharibi.

Hivi sasa, nchi nyingi za Kiafrika zinakabiliwa na matatizo ya chakula, hatari ya njaa, kuongezeka umaskini na ukosefu wa ajira. Hali hiyo imepelekea baadhi ya watu kuvutiwa na makundi ya kigaidi na hivyo kuzidisha matatizo ya kiusalama barani humo. Mataifa makubwa ya Magharibi yanajaribu kuongeza ushawishi wao katika bara la Afrika kwa kutumia vibaya matatizo hayo.
William Gumede, Mkurugenzi wa Taasisi ya Democracy Works, anasema kuhusu safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani barani Afrika: "Inaonekana kuwa vita baridi vipya vimeanza kudhihiri barani Afrika."
Vita ambavyo bila shaka matokeo yake yatayaathiri mataifa ya Afrika.