Ripoti: Mikusanyiko ya Wakristo yachangia kuenea surua Zimbabwe
(last modified Tue, 16 Aug 2022 02:41:58 GMT )
Aug 16, 2022 02:41 UTC
  • Ripoti: Mikusanyiko ya Wakristo yachangia kuenea surua Zimbabwe

Wizara ya Afya ya Zimbabwe imetangaza kuwa, mlipuko wa ugonjwa wa surua nchini humo umesababishwa na mikusanyiko ya kidini ya Wakristo.

Ripoti ya Wizara ya Afya inaeleza hayo katika hali ambayo, ugonjwa wa surua uliolipuka nchini humo kuanzia Aprili mwaka huu unaelezwa kuwa, umeshasababisha vifo vya makumi ya watoto.

Taarifa ya Wizara ya Afya ya Zimbabwe imesema kwamba, mlipuko huo sasa umesambaa kote nchini humo na kusababisha asilimia 6.9 ya vifo miongoni mwa walioambukizwa.

Vifo vya watoto 80 vimesharipotiwa hadi sasa nchini Zimbabwe na kuzua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wananchi.

Waziri wa Afya Jasper Chimedza amesema kwamba, kufikia Alkhamisi wiki iliyopita, kulikuwa na kesi 1,036 zilizoshukiwa kuwa za surua, wakati 125 zikithibitishwa tangu kutokea kwa mlipuko huo.

Watoto wakipatiwa chanjo ya Surua

 

Jimbo la Manicaland mashariki mwa Zimbabwe linasemekana kuongoza kwa maambukizi. Chimedza ameongeza kusema kwamba kesi ya kwanza iliripotiwa Aprili 10 na tangu wakati huo maambukizi yameenea kote nchini, yakisemekena kuchochewa zaidi na mikusanyiko ya waumini makanisani.

Wengi walioambukizwa ni watoto wenye umri kati ya miezi 6 na 15, wengi wakitokea kwenye familia za waumini waliokataa chanjo dhidi ya surua kutokana na imani za kidini.

Baadhi ya madhehebu nchini Zimbabwe huwakataza wafuasi wao kupokea aina yoyote ile ya chanjo au matibabu. Madhehebu hayo yana mamilioni ya wafuasi wanaoamini miujiza ya uponyaji pamoja na kujikwamua kutoka kwenye umaskini.