Mripuko wa surua umeua watoto 700 nchini Zimbabwe
Mripuko wa surua umeua takriban watoto 700 nchini Zimbabwe tokea mwezi Aprili mwaka huu hadi sasa.
Wizara ya Afya ya Zimbabwe imeeleza katika taarifa yake kwamba, kufikia Septemba 4 mwaka huu, kesi 6,291 za maradhi hayo zilikuwa zimeripotiwa, mbali na vifo 698.
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, katika kipindi cha kuanzia Aprili mwaka huu hadi Septemba 4, watu 4,459 waliokuwa wamekumbwa na maradhi hayo wamepata afueni.
Wizara ya Afya ya Zimbabwe imesema, asilimia 47.8 ya kesi za maradhi hayo zimeripotiwa katika mkoa wa Manicaland mashariki mwa Zimbabwe, huku mkoa wa Mashonaland Magharibi ukirekodi vifo vingi, asilimia 16.5 ya vifo vimeripotiwa hadi sasa nchini humo.

Serikali ya Zimbabwe imesema itaongeza juhudi za utoaji chanjo pamoja na kutumia sheria ya muda itakayoiruhusu kutumia fedha kutoka mfuko wa kitaifa wa dharura, ili kukabiliana na janga hilo.
Habari zaidi zinasema kuwa, akthari tya walioambukizwa ni watoto wenye umri kati ya miezi 6 na 15, wengi wakitokea kwenye familia za waumini waliokataa chanjo dhidi ya surua kutokana na imani za kidini.