Sep 28, 2022 08:09 UTC
  • DRC yatangaza kumalizika mripuko wa sasa wa Ebola

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza habari ya kutokomezwa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa nchi.

Katika taarifa jana Jumanne, Waziri wa Afya wa DRC, Jean-Jacques Mbungani Mbanda amesema kuwa mripuko wa sasa wa virusi vya Ebola katika mkoa wa Kivu Kaskazini umemalizika. 

Aidha Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha habari ya kumalizika kwa mripuko huo wa Ebola, likisisitiza kuwa ndio uliokuwa wa kiwango cha chini kabisa kwa kuwa kesi moja ya maradhi hayo ndiyo iliyonakiliwa.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, Kongo DR ilizindua kampeni ya kutoa chanjo katika mji Beni, mashariki mwa nchi, baada ya kesi ya virusi hivyo kuthibitishwa katika mji huo.

Hadi sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa na miripuko 15 ya Ebola tangu mwaka 1976, ambapo kati ya hiyo, saba imekumba nchi hiyo tangu mwaka 2018.

Kampeni ya chanjo mashariki ya DRC

Haya yanajiri huku idadi ya watu walioaga dunia nchini Uganda kwa maradhi hayo hatari ikiongezeka na kufikia 23, wakati huu ambapo kuna na taarifa za kuenea kwa kasi maambukizo ya maradhi hayo nchini humo.

Ebola ni ugonjwa hatari ambao unaweza kusababisha kifo na hupata binadamu na nyani. Ikumbukwe kuwa, mripuko mkubwa zaidi wa ugonjwa hatari wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za Guinea, Liberia na Sierra Leone huko magharibi mwa bara la Afrika. 

Tags