Jun 13, 2016 02:48 UTC
  • Wakimbizi 10 hupoteza maisha kila siku nchini Nigeria

Duru za kieneo nchini Nigeria zimeeleza kuwa wakimbizi 10 hufariki dunia kila siku katika kambi ya wakimbizi nchini humo.

Taarifa iliyotolewa Jumapili ya jana imeongeza kuwa, kwa kila siku wakimbizi 10 hupoteza maisha yao katika kambi ya wakimbizi ya Banki, kaskazini mashariki mwa Nigeria. Kwa mujibu wa ripoti hiyo wakimbizi hao ambao waliokoka mashambulizi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram, hupoteza maisha kwa namna ya kutisha katika kambi hiyo. Kijana mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe amenukuliwa akisema kuwa, katika makaburi ya Bulashira, kuna makaburi mapya yapatayo 376 ambamo wamezikwa wakimbizi hao ndani ya kipindi cha miezi mitatu pekee iliyopita.

Kambi ya wakimbizi ya Banki, ipo umbali wa kilometa 130 mashariki mwa mji wa Maiduguri mji mkubwa wa jimbo la Borno, na katika mji mdogo ulio karibu na mpaka wa nchi hiyo na Cameroon.

Sababu kuu inayosababisha vifo vya wakimbizi hao inatajwa kuwa ni uhaba wa chakula kwenye kambi hiyo.

Tags