UN: Wahutu 21 wameuawa katika mapigano nchini DRC
Umoja wa Mataifa umesema kwa akali watu 21 wameuawa na wengine zaidi ya 40 wamejeruhiwa katika mapigano yaliyolenga waasi wa Kihutu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Amouzoun Codjo Martin, amesema mauaji hayo yalifanywa na makundi mawili ya wabeba silaha katika kijiji cha Mukeberwa, mkoa wa Kivu Kaskazini. Msemaji huyo wa UN ameyataja makundi hayo kuwa UPDI na NDC.
Habari zaidi zinasema kuwa, mbali na mauaji hayo, makumi ya nyumba zimeteketezwa katika mashambulizi hayo ya kuvizia.
Wiki iliyopita, Kamanda mwandamizi wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo alisema waasi wa Kinyarwanda wa FDLR wametimuliwa kutoka maeneo kadhaa ya mashariki mwa nchi hiyo. Kapteni Guillaume Ndjike Kaiko ambaye ndiye msemaji wa oparesheni ya jeshi la DRC ijulikanayo kama Sokola 2 katika mkoa wa Kivu Kaskazini alisema katika kipindi cha wiki moja iliyopita jeshi limewatimua waasi wa FDLR kutoa katika maeneo ya Libero, Walikale, Buleusa, Rusamambo, Mizinga na Rusoha.
Eneo la mashariki mwa DRC halina usalama kwa takriban miongo miwili sasa na limekuwa likishuhudia harakati za makundi mbalimbali ya uasi. Baadhi ya makundi hayo yamevivamia na kuvikalia vijiji vya eneo hilo na kusababisha wakazi wa vijiji hivyo kubaki bila ya makazi.