UNHCR: Katika kufunga kambi ya wakimbizi Kenya ichunge misingi ya ubinaadamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9163-unhcr_katika_kufunga_kambi_ya_wakimbizi_kenya_ichunge_misingi_ya_ubinaadamu
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), ameitaka serikali ya Kenya kuheshimu misingi ya ubinaadamu katika mwenendo mzima wa kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 14, 2016 03:02 UTC
  • UNHCR: Katika kufunga kambi ya wakimbizi Kenya ichunge misingi ya ubinaadamu

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), ameitaka serikali ya Kenya kuheshimu misingi ya ubinaadamu katika mwenendo mzima wa kufunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini humo.

Filippo Grandi aliyasema hayo jana mwishoni mwa safari yake ya siku tano nchini Kenya na Somalia na kuongeza kuwa, ikiwa serikali ya Nairobi imeazimia kuwarejesha nyumbani wakimbizi hao kutoka kambi ya Dadaab, basi lazima shughuli hiyo ifanyike kwa namna inayostahili na kuchunga misingi ya ubinaadamu na sheria za kimataifa. Kadhalika aliongeza kuwa, asilimia kubwa ya wakimbizi wa Kisomali walioko nchini Kenya wana wasiwasi mkubwa wa kurejea nchini kwao kutokana na kuendelea mauaji ya kila mara ndani ya nchi hiyo ya pembe ya Afrika. Kambi ya Dadaab iko umbali wa kilomita 100 katika mpaka wa pamoja wa Kenya na Somalia, huku ikiwa ndio kambi kubwa kabisa ya wakimbizi duniani. Serikali ya Nairobi imeazimia kuifunga kambi hiyo kutokana na sababu za kiusalama. Kwa mujibu wa serikali hiyo, karibu miaka 25 iliyopita, zaidi ya wakimbizi laki sita wamekuwa wakiishi nchini Kenya huku mahitaji yao yakidhaminiwa na serikali ya nchi hiyo suala ambalo limekuwa likilemaza uchumi na usalama wake. Hii ni katika hali ambayo hivi karibuni pia Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Filippo Grandi, alinukuliwa akisema kuwa, serikali ya Kenya inapaswa kulegeza msimamo wake kuhusu muda wa mwisho ilioutoa kwa ajili ya kuwarejesha makwao wakimbizi wapatao 350,000 Wasomali walioko nchini humo.