Jitihada za Uhuru zimezaa matunda; waasi wa M23 wakubali kuondoka Kivu Kaskazini
Juhudi za Rais wa zamani wa Kenya Uhuru Kenyatta za kurejesha amani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimepiga hatua kubwa kufuatia waasi wa M-23 kukubali kuondoka katika eneo hilo lililoathiriwa na machafuko.
Haya yamebainika jana baada ya Uhuru kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi ya juu wa kisiasa na kijeshi wa kundi la waasi wa M-23 huko Mombasa, Kenya yeye akiwa kama mpatanishi wa mchakato wa amani wa Afrika mashariki huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano kati ya Uhuru Kenyatta na viongozi wa M-23 imeeleza kuwa, katika kudhihirisha nia njema na azma ya kupatia ufumbuzi hali ya mambo huko Kivu Kaskazini,viongozi wa waasi wa M-23 wamekubali kuendelea kuondoka kwa mpangilio katika jimbo hilo na kuheshimu ustishaji vita.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, waasi wa M-23 aidha wamekubali kuheshimu na kushirikiana na kikosi cha kulinda amani cha kikanda cha Afrika Mashariki; ambapo sasa kikosi hicho kimeanza kuchukua maeneo yaliyokuwa yakishikiliwa na waasi hao.

Hadi kufikia sasa Uhuru Kenyatta amefanikisha mazungumzo matatu ya mapatano ya amani jijini Nairobi kati ya waasi na serikali ya Kinshasa; ambapo mazungumzo ya nne yamepangwa kufanyika katikati ya mwezi Februari mwaka huu.
Waasi wa M-23 wamemshukuru Uhuru Kenyatta kwa azma yake endelevu ya kutafuta msaada wa kimataifa na ushirikiano kwa lengo la kurejesha amani mashariki mwa Kongo na kuwapunguzia mateso raia wa eneo hilo.