Dec 25, 2022 07:39 UTC
  • Mapigano ya kikabila yaua watu wengine 7 Darfur, Sudan

Mapigano ya kikabila yaliyozuka katika eneo la Darfur nchini Sudan yamesababisha vifo vya saba, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Shirika la habari la Sudan SUNA liliripoti habari hiyo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, mapigano hayo baina ya wafugaji Waarabu na wakulima wa kabila la Daju yametokea katika mji wa Nyala, makao makuu ya jimbo la Darfur Kusini.

Haijabanika mara moja sababu za kutokea mapigano hayo mapya ya kikabila baina ya Waarabu na wasio Waarabu katika eneo la Darfur ambalo hushuhudia mapigano ya kikabila mara kwa mara.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, watu wasiopungua 20 walilazwa katika hospitali ya Nyala baada ya kujeruhiwa katika mapigano hayo yaliyoanza tokea Jumatano iliyopita.

Mwezi uliopita wa Novemba, mapigano mengine ya kikabila yaliripotiwa katika eneo hilo la Darfur huko Sudan na kusababisha vifo vya karibu watu 24 na kupelekea hali ya dharura kutangazwa eneo hilo.

Mapigano yanashuhudiwa Darfur licha ya uwepo wa walinda amani wa UN

Aidha mwezi mmoja kabla ya hapo, watu wasiopungua 230 waliuawa huku wengine zaidi ya 200 wakijeruhiwa katika mashambulizi ya dhidi ya vijiji kadhaa vya jimbo la Blue Nile, kusini magharibi mwa Sudan.

Mapigano haya ya hivi sasa ni wimbi jipya la ghasia za kikabila ambazo zimeenea kote nchini Sudan licha ya kutiwa saini mkataba wa amani wa nchi nzima miaka miwili iliyopita.

Tags