Mkutano wa ahadi wa kusaidia Bonde la Ziwa Chad umeanza nchini Niger
Serikali za Niger, Ujerumani na Norway, pamoja na Umoja wa Mataifa zinashiriki kwa pamoja mkutano wa tatu wa ngazi ya juu kuhusu Kanda ya Bonde la Ziwa Chad, ambao ulianza jana na kuendelea leo katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Mahatma Gandhi katika mji mkuu wa Niger, Niamey.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA tangu mkutano wa mwisho uliofanyika Berlin Ujerumani mwaka 2018, mgogoro katika bonde la ziwa Chad umezidi kuwa mbaya kwa kuongezeka vurugu, upungufu wa maendeleo, mahitaji ya kibinadamu, vikwazo vya upatikanaji wa huduma za msingi za kijamii, mifumo ya uzalishaji na usaidizi wa kibinadamu na matokeo yake watu milioni 5.3 wamesalia bila makazi katika eneo hilo.
Shirika hilo limeongeza kuwa matokeo ya pamoja ya kuongezeka kwa ukosefu wa utulivu, athari za muda mrefu za janga la COVID-19, athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga ya kiuchumi yamezidisha hali mbaya ya kibinadamu.
Katika mkutano huo wa ahadi nchi za pembezoni zimesisitiza dhamira yao isiyoyumba katika kushughulikia changamoto hizo tata ikiwa ni pamoja na kupambana na ugaidi na itikadi kali za kivita.
OCHA inasema maendeleo yaliyopatikana yanadhihirisha kuwa changamoto kubwa ya watu kulazimika kufurushwa inaweza kukomeshwa.
Mahitaji ya fedha kwa ajili ya kukabiliana na dharura katika bonde la ziwa Chad yameongezeka kwa dola za Marekani milioni 259 tangu mwaka 2018.
Mahitaji ya ufadhili wa uimarishaji yanakadiriwa kuwa dola za bilioni 1.8.
Eneo la ziwa Chad ni mojawapo ya maeneo yenye mazingira ya migogoro na migogoro ya muda mrefu zaidi duniani.
Licha ya baadhi ya matukio chanya, viwango vya juu vya vurugu vinaendelea kuwa na athari mbaya kwa mamilioni ya watu nchini Cameroon, Chad, Niger na Nigeria.../