Mripuko wa bomu waua makumi ya watu katikati ya Nigeria
Wafugaji 27 wa kabila la Fulani wamepoteza maisha huku wengine wengi wakijeruhiwa, baada ya bomu kuwaripukia katika kijiji cha Rukubi, katika mpaka wa majimbo ya Nasarawa na Benue, katikati ya Nigeria.
Msemaji wa Polisi katika jimbo la Nasarawa, Ramhan Nansel amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, kamandi ya polisi katika eneo hilo imeanzisha uchunguzi kubaini kiini cha mripuko huo, ili kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wake.
Naye Gavana wa jimbo la Nasarawa, Abdullahi Sule amesema vyombo vya dola vinafanya juu chini kuhakikisha kuwa waliohusika na umwagaji damu huo wanakabiliwa na mkono wa sheria.
Amewataka watu wa kabila la Fulani kuwa watulivu, na wajizuie kuchukua hatua yoyote ya ulipizaji kisasi. Amebainisha kuwa, maafisa usalama wametumwa katika eneo hilo ili kuchunguza chanzo cha shambulio hilo la Jumatano.
Haya yanajiri siku chache baada ya genge la watu wenye silaha nchini Nigeria kushambulia kijiji kimoja na kuwaua watu wasiopungua 12 katika shambulizi jipya huko kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo.
Ukosefu wa usalama umeongezeka sana nchini Nigeria hivi sasa, wakati nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ikikaribia kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwezi Februari mwaka huu 2023.