Papa alaani ukoloni wa kiuchumi barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i93580-papa_alaani_ukoloni_wa_kiuchumi_barani_afrika
Jumanne wiki hii, katika siku ya kwanza ya safari yake Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Papa Francis, kiongozi wa Wakatoliki duniani, amelaani vikali "ukoloni wa kiuchumi" unaotekelezwa barani Afrika na hasa katika nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 02, 2023 09:15 UTC
  • Papa alaani ukoloni wa kiuchumi barani Afrika

Jumanne wiki hii, katika siku ya kwanza ya safari yake Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Papa Francis, kiongozi wa Wakatoliki duniani, amelaani vikali "ukoloni wa kiuchumi" unaotekelezwa barani Afrika na hasa katika nchi hiyo.

Akizungumza katika mkusanyiko wa viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika ikulu ya rais wa nchi hiyo, Papa Francis amesema: "Ondoa mikono yako kutoka Kongo na Afrika. Acheni kuinyonga Afrika. Afrika si mgodi wa kuporwa na hakuna ardhi ya kupora."

Papa Francis ameashiria karne kadhaa za ukoloni mkubwa na wa kina wa ardhi za Kiafrika na ukoloni ambao ulitekelezwa na madola ya Magharibi ambapo matokeo yake mabaya  bado yanaendelea kuzidhuru nchi za Kiafrika licha ya miongo kadhaa ya uhuru.

Nchi za Ulaya, haswa Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji, Italia na Ujerumani zina historia ya karne kadhaa katika kukalia kwa mabavu ardhi za Afrika, kuua Waafrika kwa umati na kupora utajiri wa maeneo yote ya bara hilo. Ukoloni wa Wazungu katika maeneo yaliyokuwa chini ya udhibiti wao uliambatana na vitendo vya kikatili, ukandamizaji mkubwa wa wenyeji, utumwa wa watu wa Kiafrika, uporaji mkubwa wa maliasili hasa madini, kuwatumukisha wenyeji kwa lazima na mambo mengine mengi yasiyo ya kibinadamu.

Wakati wa kukoloniwa bara la Afrika, mamilioni ya wenyeji wa Kiafrika walitumwa kama watumwa katika nchi zingine huku wakisafirishwa katika mazingira magumu sana. Waafrika walipelekwa kwa lazima kama watumwa katika nchi zilizokuwa chini ya ukoloni wa Ulaya, ikiwa ni pamoja na Amerika Kaskazini na Amerika ya Kusini. Wakati huo huo, wakoloni wa Ulaya walipata faida ya mabilioni ya dola kutokana na biashara ya kikatili ya utumwa na hivyo fedha za utumwa ndio msingi wa utajiri wa nchi nyingi za Ulaya na pia Marekani na Kanada.

Hata hivyo, katika karne ya 20, zama za ukoloni wa kitambo zilifikia mwisho na nchi za Magharibi, hasa za Ulaya, zinajua fika kwamba haiwezekani tena kuendeleza uhusiano uliokuwepo wakati wa ukoloni na nchi za Kiafrika ambazo zilikuwa makoloni yao. Kwa sababu hiyo, nchi za kikoloni kama Ufaransa na Uingereza ikiwemo Marekani, ambayo  ni kinara wa nchi za Magharibi, zinajaribu kuendeleza ukoloni mamboleo kwa sura nyingine na kudumisha ushawishi wao katika nchi za Kiafrika kwa kuzingatia maslahi yao na kuendelea kupora utajiri wa nchi hizo.

Miongoni mwa visingizio vipya vya nchi za Ulaya kuendelea kuwepo katika nchi za Kiafrika ni suala la eti kupambana na ugaidi ambalo Ufaransa hasa imelitumia vibaya ili kuendelea kupora rasilimali na migodi ya nchi za ukanda wa Sahel ambapo hasa inalenga kupora madini muhimu ya urani na dhahabu.

Ingawa nchi za Kiafrika zilipata uhuru katika kipindi cha baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Wamagharibi daima wamejaribu kudumisha na kuimarisha ushawishi wao wa kisiasa na kiuchumi katika bara hili kwa kuathiri mifumo ya kisiasa, kiuchumi na hata kijeshi ya nchi hizo. Rais wa Russia Vladmir Putin anasema: Tunashuhudia kwamba baadhi ya nchi za Magharibi zinakabiliana na serikali za Afrika kwa kutumia mashinikizo, vitisho na ulaghai. Kwa njia hizo, zinajaribu kurejesha ushawishi na utawala wao juu ya makoloni yao ya zamani, kwa kutumia mbinu mpya.

Rais Putin wa Russia

Lakini, katika miaka ya hivi karibuni, pamoja na mabadiliko ya kimsingi katika muundo wa uchumi wa ulimwengu na kuibuka madola mapya yenye nguvu za kiuchumi, ushawishi wa nchi za Magharibi katika  nchi za Kiafrika umepungua, na katika hali hii, nchi zinazoibuka kiuchumi ulimwenguni kamakama vile China, India, Brazil na Russia, ni washirika wakuu wapya wa kibiashara wa nchi za Afrika.

Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia anasema: Marekani na nchi za Ulaya, ambazo zinataka kusitishwa kwa ushirikiano wa nchi za Kiafrika na Russia, kwa hakika zinataka kurejesha utegemezi wa kikoloni wa Wamagharibi kwa madhara ya nchi za Afrika.

Katika hali ya sasa, kutokana na uwezo wa kibinadamu na wa kimaumbile na vile vile kutokana na kuwa na akiba kubwa ya utajiri wa nishati na madini, nchi za Afrika zinazidi kupata ushawishi kimataifa na sasa zinakodolewa macho ya tamaa na madola ya kibeberu ya Magharibi.