Zimbabwe inapoteza madaktari na walimu kwa unafiki wa Uingereza
(last modified Thu, 09 Feb 2023 02:18:43 GMT )
Feb 09, 2023 02:18 UTC
  • Zimbabwe inapoteza madaktari na walimu kwa unafiki wa Uingereza

Uingereza ambayo sasa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa wauguzi na walimu baada ya kujitoa katika Umoja wa Ulaya, imekuwa ikijielekeza katika koloni lake la zamani, Zimbabwe kutafuta wafanyakazi wa sekta ya umma wakiwemo wauguzi, madaktari na walimu.

Wauguzi na madaktari zaidi ya 4,000 wameondoka Zimbawe tangu mwezi Februari mwaka juzi wa 2021. Nchi ambayo kwa sasa inakimbiliwa pakubwa na sekta ya wauguzi na madaktari kutoka Zimbabwe ni Uingereza. Takwimu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza zinaonyesha kuwa Zimbabwe sasa ni kati ya nchi tano kuu ambayo wafanyakazi wao wenye ujuzi na weledi wanapatiwa viza kwa ajili ya kufanya kazi nje ya nchi. 

Chama cha Madaktari wa Zimbabwe kimeeleza kuwa, nchi hiyo ina madaktari 3,500 wanaopaswa kutoa huduma kwa watu milioni 15. Zimbabwe pia inakabiliwa na upungufu wa wauguzi ambapo mwaka 2017 takwimu za Benki ya Dunia zilionyesha kuwa wauguzi 2 walikuwa wakitoa huduma kwa wagonjwa elfu mmoja nchini humo. 

Licha ya migomo inayoikabili sekta ya afya ya Uingereza lakini nchi hiyo bado ina idadi ya kutosha ya wauguzi. Uwiano wa wauguzi wa Uingereza wa hivi sasa umetajwa kuwa katika kiwango cha 8.5 kwa kila watu elfu moja yaani mara tatu zaidi ya idadi ya wauguzi nchini Zimbabwe. Hii ni katika hali ambayo Uingereza hutumia kiasi cha dola 281,000 kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa kila daktari nchini humo. 

Si katika sekta ya wauguzi na madaktari pekee, bali Uingereza hivi sasa inawabembeleza pia walimu kutoka Zimbabwe kwenda kufundisha nchini humo. Kuanzia mwezi Februari mwaka huu Zimbabwe inaazimia kujiunga na kundi teule la mataifa na maeneo ambayo walimu wenye ujuzi kutoka nchi hizo watastahiki kupata Hadhi ya Walimu Waliohitimu (QTS) ambayo itawaruhusu kufanya kazi kwa muda mrefu huko Uingereza.

Uingereza sasa yajielekeza kuwasaka walimu kutoka Zimbabwe