Mkutano wa viongozi wa Afrika kuanza leo, mpango wa "Kunyamazisha Bunduki" unajadiliwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i94174-mkutano_wa_viongozi_wa_afrika_kuanza_leo_mpango_wa_kunyamazisha_bunduki_unajadiliwa
Mkutano wa 36 wa viongozi wa nchi za Afrika unaanza leo Jumamosi, katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kujadili masuala kadhaa hasa maendeleo yaliyopatikana katika kampeni ya "Kunyamazisha Bunduki" na changamoto za usalama wa chakula barani Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 18, 2023 00:03 UTC
  • Mkutano wa viongozi wa Afrika kuanza leo, mpango wa

Mkutano wa 36 wa viongozi wa nchi za Afrika unaanza leo Jumamosi, katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, kujadili masuala kadhaa hasa maendeleo yaliyopatikana katika kampeni ya "Kunyamazisha Bunduki" na changamoto za usalama wa chakula barani Afrika.

Mkutano huo pia utajadili masuala ya kisiasa na kiuchumi sambamba na mada kuu ya mwaka huu, ambayo inajadiliwa chini ya anwani "Kuharakisha Utekelezaji wa Eneo la Biashara Huria la Bara". Viongozi wa Afrika pia watatathmini mpango wa utekelezaji wa miaka kumi ya kwanza na kubuni mpango wa pili wa utekelezaji wa miaka kumi nyingine wa dira ya Umoja wa Afrika hadi 2063.

Rais wa Senegal, Macky Sall, ambaye anashikilia uenyekiti wa Umoja wa Afrika tangu Februari 2022, atakabidhi nafasi hiyo kwa Rais wa Comoro, Azali Assoumani.

Shughuli za mkutano huo zilianza hapo kabla katika makao makuu ya Umoja wa Afrika kwa kikao cha kawaida cha 42 cha Baraza la Utendaji la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Umoja huo.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki, amesema Umoja huo umefanikiwa katika juhudi zake za kuimarisha amani katika nchi kadhaa za bara hilo, jambo linaloashiria kuwa jumuiya hiyo ya Afrika imedhamiria kutoa kipaumbele kwa masuluhisho ya amani yanayopaswa kusimamiwa na Waafrika wenyewe.

Faki ameongeza kuwa umoja huo ulichangia pakubwa katika maridhiano ya pande hasimu katika nchi za Ethiopia na Sudan, na kusema kuwa licha ya uingiliaji wa kigeni katika masuala ya nchi hizi, AU imechangia katika hatua za kuelekea kwenye mtazamo mpya, wa kina na wa maelewano."

Pamoja na hayo yote wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama na kisiasa, wakieleza kuwa juhudi za Afrika kuhusu mpango wa "Kunyamazisha Bunduki" bado ziko mbali.