Wananchi wa Nigeria wapiga kura kuchagua Rais mpya na Wabunge
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i94438-wananchi_wa_nigeria_wapiga_kura_kuchagua_rais_mpya_na_wabunge
Mamilioni ya wapigakura nchini Nigeria wameelekea katika masanduku ya kupigia kura leo Jumamosi kushiriki uchaguzi wa rais wenye mchuano mkali, kumtafuta mrithi wa Muhammadu Buhari, ambaye anamaliza mihula yake miwili ya uongozi.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Feb 25, 2023 03:48 UTC
  • Wananchi wa Nigeria wapiga kura kuchagua Rais mpya na Wabunge

Mamilioni ya wapigakura nchini Nigeria wameelekea katika masanduku ya kupigia kura leo Jumamosi kushiriki uchaguzi wa rais wenye mchuano mkali, kumtafuta mrithi wa Muhammadu Buhari, ambaye anamaliza mihula yake miwili ya uongozi.

Kati ya wagombea wote 18, mchuano mkali unatazamiwa kuwa baina ya mgombea wa chama tawala cha All Progressives Congress (APC), ambaye pia ni gavana wa zamani wa Lagos, Bola Ahmed Tinubu, na makamu wa rais wa zamani wa Nigeria, Atiku Abubakar wa chama kikuu cha upinzani cha People's Democratic Party (PDP).

Hii ni mara ya sita katika kipindi cha miongo mitatu ambapo Atiku Abubakar anawania urais nchini Nigeria. Alikuwa Makamu wa Rais wakati wa utawala wa Rais Olusegun Obasanjo hadi mwaka 2007.

Mgombea wa chama wa Leba, Peter Obi anatazamwa kama mwanasiasa wa 'pembeni' na mwanagenzi katika siasa za nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika, ingawaje pia ana umaarufu. 

Wanigeria zaidi ya milioni 90 wamesajiliwa kuwa wapigakura, na wametimiza masharti ya kushiriki zoezi hilo. Mbali na kuchagua rais, Wanigeria pia wanapiga kura ya kuchagua watunga sheria, yaani Wabunge 360 na Maseneta 109.

Wagombea wakuu wa uchaguzi wa rais nchini Nigeria

Iwapo hakuna mgombea ataibuka mshindi katika uchaguzi wa rais, mchuano huo utaingia katika duru ya pili inayopasa kufanyika katika kipindi kisichozidi wiki tatu.

Uchumi uliozorota na kero la magenge ya kigaidi haswa kundi la Boko Haram ni miongoni mwa masuala muhimu ambayo Wanigeria wanataka yapatiwe ufumbuzi na serikali ijayo.

Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta anaongoza timu ya waangalizi wa Umoja wa Afrika kwenye uchaguzi huo. Kenyatta na waangalizi wenzake wa AU wanasema wanaamini kuwa, demokrasia itadumishwa na kulindwa nchini Nigeria katika kipindi hiki cha uchaguzi na hata baada ya zoezi hilo.