Kampuni ya Taifa Gas ya Tanzania kujenga kiwanda cha gesi Kenya
Kampuni ya gesi ya kupikia, Taifa Gas yaTanzania imeanzisha rasmi ujenzi wa kiwanda na ghala ya kuhifadhi gesi ya kupikia ya tani elfu 45, katika eneo maalumu la kiuchumi karibu na bandari ya Mombasa, Kenya.
Kiwanda hicho cha mabilioni ya fedha kitagharimu dola milioni 200. Taifa Gas itatoa ushindani wa kibiashara na kampuni ya Africa Gas and Oil Limited (AGOL) yenye kiwanda cha tani elfu 25, kinachomilikiwa na Mohammed Jaffar, Mombasa.
Akizindua rasmi ujenzi huo kwa kuweka jiwe la msingi, Rais William Ruto wa Kenya, amesema kuwa, kama serikali wanaunga mkono mradi huo ambao sio tu kwa manufaa ya Kenya bali kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mbali na nafasi za ajira na kuinua uchumi, pia utachangia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kwa kupunguza utumiaji wa kuni na makaa kwa kupikia na badala yake kutumia nishati safi isiyoharibu mazingira.
“Asilimia 70 ya Wakenya wanatumia kuni na makaa kwa upishi, hii sio tu kuwadhuru afya yao bali pia inachangia uharibifu wa misitu. Uzalishaji wa gesi safi utawasaidia wakenya kupata gas kwa bei nafuu na mazingira salama,” amesema Rais William Ruto.
Mwenyekiti wa kampuni ya Taifa Gas, Rostam Aziz, ameipongeza serikali ya Kenya kukubali kuwekeza katika taifa hilo amesema kuwa, awali alikuwa amelenga kujenga kiwanda na ghala ya kuhifadhi tani elfu 30 lakini rais akaongeza hadi tani elfu 45. Akigusia vikwazo vya uwekezaji katika mataifa ya Afrika, Aziz amewasihi marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuondoa kodi na vikwazo mipakani ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuwa huru kuwekeza katika bara lao badala ya kutoa mwanya kwa mataifa kama China kuwekeza kwa urahisi na kuwawekea vikwazo wa Afrika wenyewe.