Mar 24, 2023 02:23 UTC
  • Ripoti: Vifo vya hujuma za kigaidi eneo la Sahel vimeongezeka kwa 2000%

Ripoti mpya iliyochapishwa na taasisi moja inayofuatilia mashambulizi na mieiendo ya makundi ya kigaidi duniani inasema kuwa, vifo vinavyotokana na hujuma za kigaidi katika eneo la Sahel barani Afrika vimeongezeka kwa asilimia 2000 katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Ripoti hiyo iliyochapishwa na taasisi ya Institute for Economics and Peace yenye makao yake Australia imeeleza kuwa, eneo la Sahel katika chini ya jangwa la Sahara barani Afrika ndicho kitovu cha ugaidi hivi sasa duniani.

Imesema eneo hilo lilisajili vifo vingi vilivyotokana na hujuma za kigaidi mwaka jana 2022, kuliko vifo vilivyorekodiwa kwa ujumla katika maeneo ya Asia Kusini, Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu wasiopungua 22,074 wameuawa katika mashambulizi 6,408 ya kigaidi katika eneo la Sahel barani Afrika baina ya mwaka 2007 na 2022. Utafiti wa Institute for Economics and Peace umefichua kuwa, Burkina Faso ndiyo iliyonakili vifo vingi vya hujuma za kigaidi, ambapo watu 1,135 waliuawa mwaka jana, ikilinganishwa na 759 mwaka juzi.

Magaidi wa Daesh nchini Burkina Faso

Kabla ya hapo, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua zaidi kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya ugaidi katika eneo la Sahel barani Afrika.

Vifo hivyo vimeripoti katika hali ambayo, nchi 5 za eneo la Sahel Afrika linalojumuisha nchi za Burkina Faso, Mali, Mauritania, Niger na Chad kwa muda sasa zinaendesha operesheni kubwa dhidi ya makundi ya kigaidi katika ukanda huo.

Takwimu za Shirika la Kuhudumi Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) zinaonesha kuwa, mgogoro wa usalama katika eneo la Sahel mbali na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha, lakini pia umewakosesha makazi zaidi ya watu milioni 2.5 katika muda wa muongo mmoja uliopita.

Tags