Maelfu wakimbia Sudan huku usitishaji mapigano ukigonga mwamba
(last modified Thu, 20 Apr 2023 12:25:07 GMT )
Apr 20, 2023 12:25 UTC
  • Maelfu wakimbia Sudan huku usitishaji mapigano ukigonga mwamba

Maelfu ya wananchi wa Sudan wanakimbia mapigano yanayoendelea nchini humo leo yakiingia katika siku ya sita baada ya kugongwa mwamba jitihada za kusitisha mapigano. Hii ni mara ya pili ambapo usitishaji vita unakiukwa huko Sudan kati ya jeshi la taifana kundi lenye nguvu la wanajeshi wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF).

Maelfu ya wakazi wa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, wamekimbia makazi yao wakihofia mapigano hayo. Ripoti zinasema hadi sasa wanajeshi 320 waliokimbia mapigano Sudan wamezuiwa katika nchi jirani ya Chad. 

Khartoum na mapigano makali ya pande hasimu 

Wanajeshi hao wa Sudan waliotoroka mapigano makali nchini mwao walivuka mpaka siku ya  ya Jumapili na kujisalimisha kwa jeshi la Chad. Haya ni kwa mujibu wa Bichara Issa Djadallah Waziri wa Ulinzi wa Chad.

Watu zaidi ya 330 wameuawa katika mapigano yanayoendelea huko Sudan kati ya pande hasimu huku wengine zaidi ya 3,200 wakijeruhiwa. Haya yameelezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Ujerumani na Japan pia zinajiandaa kuwarejesha nchini raia wao walioko Sudan.  

Siku nzima ya Jumatano, pande  mbili hasimu zilipigana kuzunguka makao makuu ya kijeshi katikati mwa Khartoum, ambayo wanajeshi wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF) wamejaribu kuyateka mara kadhaa pamoja na uwanja wa ndege ulipo karibu na eneo hilo.

Umoja wa Mataifa ulipanga kukutana leo na wawakilishi wa Umoja wa Afrika (AU) na wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) kujadili hali ya mambo ya Sudan. 

Tags