WHO yatahadharisha kuhusu hali mbaya ya kiafya nchini Sudan
Msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) katika eneo la Mashariki ya Mediterania ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kiafya nchini Sudan kufuatia miapigano yanayoendelea baina ya makundi mawili ya jeshi la nchi hyo.
Msemaji wa Shirika la Afya Duniani ameiambia televisheni ya Al Jazeera ya Qatar kwamba hali ya afya nchini Sudan ni majanga matupu na ya kutisha kwa sababu sasa ni vigumu sana kwa msaada wowote kuingia nchini humo.
Afisa huyu wa WHO ameeleza kwamba Sudan inahitaji misaada ya dharura ya vifaa vya matibabu.
Vitongoji vya mji mkuu wa Sudan, Khartoum, mapema leo vimeanza siku za kwanza za Idul Fitr kwa sauti za risasi na mabomu ya ndege za kivita na mizinga katika shambulio kubwa la Jeshi la Taifa kwenye viunga karibu vyote vya mji huo.
Kamandi ya Vikosi vya Jeshi la Taifa la Sudan imetangaza kwamba inaendesha operesheni ya nchi kavu katika jimbo lote la Khartoum, baada ya kile ilichokieleza kuwa ni "mafanikio ya oparesheni ya mashambulizi ya angani ambayo ililenga maeneo ya wapiganaji wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF) mjini Khartoum alfajiri ya leo Ijumaa."
Ripoti zinasema mizinga ya RSF ilikabiliana na ndege za kivita za Jeshi la Taifa katika anga ya mji wa Khartoum, muda mfupi baada ya pande hizo mbili hasimu kutangaza makubaliano ya kusitisha mapigano wakati wa Sikukuu ya Idul Fitr, ambayo imenza leo Ijumaa nchini Sudan na katika baadhi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, ametoa wito kwa pande zinazozozana nchini Sudan kuzingatia usitishaji vita wakati wa Sikukuu ya Idul-Fitr ili kuruhusu raia kufika maeneo salama, huku mapigano hayo yakiingia siku ya saba leo, Ijumaa.