WHO: Malaria bado ni tishio kwa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i96592-who_malaria_bado_ni_tishio_kwa_afrika
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa malaria, bado inatambuliwa kuwa tishio kwa bara la Afrika, haswa kutokana na kuongezeka usugu wa maradhi hayo kwa matibabu, licha ya chanjo zinazotolewa za kukabiliana na malaria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 23, 2023 22:01 UTC
  • WHO: Malaria bado ni tishio kwa Afrika

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa malaria, bado inatambuliwa kuwa tishio kwa bara la Afrika, haswa kutokana na kuongezeka usugu wa maradhi hayo kwa matibabu, licha ya chanjo zinazotolewa za kukabiliana na malaria.

Takwimu za hivi karibuni  za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kuwa, ugonjwa wa malaria ulisababisha vifo vya watu 619,000 dunianiu mwaka 2021.

WHO inakadiria kuwa karibu watu milioni 250 wataambukizwa malaria mwaka huu. Watu milioni 247 waliambukizwa malaria mwaka 2021. Takriban nusu ya watu duniani wanaishi katika eneo ambalo liko hatarini na linaweza kuambukizwa malaria.

Watoto wachanga, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wajawazito wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupata aina kali ya malaria.

Takwimu zinaonyesha kuwa, zaidi ya nusu ya vifo vyote vya malaria duniani kote vinatokea katika nchi nne za Afrika ambazo ni: Nigeria (31.3%), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (12.6%), Tanzania (4.1%) na Niger (3.9%).

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, kwa wastani bara la Afrika linarekodi kesi milioni 200 na vifo 400,000 kwa mwaka vinavyosababishwa na ugonjwa wa malaria.

Hii ina maana kuwa, karibu asilimia 90 ya kesi za ugonjwa wa malaria zipo barani Afrika; ambapo watoto 260,000 huaga dunia kila mwaka kwa ugonjwa huo.

Malaria husababishwa na vimelea na huambukizwa kwa binadamu kupitia mbu jike aina ya Anopheles. Ingawa ugonjwa huo unaweza kuzuilika na kutibika, unaweza kusababisha kifo usipotibiwa.