Vita Sudan: WHO yasema wagonjwa wengi hawawezi kupata huduma za afya
(last modified Thu, 27 Apr 2023 11:19:34 GMT )
Apr 27, 2023 11:19 UTC
  • Vita Sudan: WHO yasema wagonjwa wengi hawawezi kupata huduma za afya

Shirika la Afya Duniani WHO linasema mapigano nchini Sudan yamepelekea wagonjwa wengi wenye magonjwa sugu, kama vile ugonjwa wa figo, kisukari na saratani, kutoweza kufikia katika vituo vya afya au dawa wanazohitaji.

Taarifa ya WHO imesema atika mji mkuu wa Khartoum, asilimia 61 ya vituo vya afya vimefungwa, na asilimia 16 pekee ndiyo vinafanya kazi kama kawaida.

Mkurugenzi wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus katika taarifa Jumatano amesema Umwagaji damu ambao tumeushuhudia kwa muda wa siku 10 zilizopita nchini Sudan ni wa kuhuzunisha, katika nchi ambayo watu wake tayari wameteseka sana katika miaka ya hivi karibuni. Tayari, vurugu hizo zimeathiri vibaya afya ya raia.”

Mbali ya idadi ya vifo na majeruhi yanayosababishwa na mzozo wenyewe, WHO inatarajia kutakuwa na vifo vingi zaidi kutokana na milipuko, ukosefu wa chakula na maji, na kukatizwa kwa huduma muhimu za afya, ikiwa ni pamoja na chanjo.

WHO pia imesema katika wiki zijazo, inakadiriwa kuwa wanawake 24,000 watajifungua, lakini kwa sasa hawawezi kupata huduma ya uzazi.

Wakati huo huo, siku ya Jumatano mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, aliafiki pendekezo Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Mashariki mwa Afrika (IGAD) la kuongeza muda wa mapatano kwa saa 72 na kutuma mjumbe wa jeshi katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba. kwa mazungumzo, taarifa ya jeshi inasema. Pendekezo hilo linapendekeza kutuma wajumbe wa pande mbili hasimu yaani Jeshi la Sudan na Kikosi cha Dharura (RSF) kwenda Juba ili kujadili maelezo zaidi.

Mahasimu wakuu Sudan, Abdel Fattah al-Burhan na Mohamed Hamdan Dagalo

Mamia wameuawa na maelfu wamejeruhiwa tangu mapigano makali yalipozuka zaidi ya siku 10 zilizopita kati ya vikosi vinavyomtii mkuu wa jeshi la Sudan Abdel Fattah al-Burhan ambaye pia ni mtawala wa nchi hiyo na naibu wake, Mohamed Hamdan Dagalo, kamanda wa kikosi chenye nguvu cha msaada wa dharura (RSF) ambaye ni maarufu kwa jina la Hemet. RSF ni kikosi chenye nguvu kilichoundwa na wanamgambo wa Janjaweed ambao kwa miaka mingi walihusika katika mapigano ya mkoa wa magharibi wa Darfur.

Shirika la Kimataifa linaloshughulikia mizozo, ICG, limesema hatua za haraka zinahitajika ili kusitisha ghasia zinazoweza kugeuka kuwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe, na kuonya kwamba hali ya kutisha ambayo wengi waliihofia nchini Sudan ndiyo inayoshuhudiwa kwa sasa. 

 

 

Tags