Mapigano makali yaripotiwa Omdurman, ndege ya abiria ya Uturuki yafyatuliwa risasi
(last modified Fri, 28 Apr 2023 11:28:10 GMT )
Apr 28, 2023 11:28 UTC
  • Mapigano makali yaripotiwa Omdurman, ndege ya abiria ya Uturuki yafyatuliwa risasi

Mapigano yamezuka tena mepama leo katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum, na milipuko imeendelea kusikika katika baadhi ya maeneo ya mji huo licha ya kuanza kutekelezwa kwa mapatano ya tano ya kusitisha vita tangu mapigano ya ndani yalipoanza kati ya Jeshi la Taifa na Vikosi vya Radiamali ya Haraka (RSF) nchini humo katikati ya mwezi huu.

Mapigano yanayoendelea baina ya pande hizi hizo mbili za jeshi la Sudan yamewalazimisha maelfu ya wananchi kukimbia makazi yao na wengie kuelekea nchi jirani kama Misri, Chad na Ethiopia.

Ripoti zinasema mapigano makali yalikuwa yakiendelea kati ya pande hizo mbili, yakishirikisha Jeshi la Anga, katika maeneo ya mashambani ya kusini mwa Omdurman.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa mamia kwa maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao nchini Sudan ili kuepuka mapigano, na kwamba kuna mamia ya maelfu ya wengine ambao bado wamekwama katika maeneo yenye mapigano makali.

Kamisheni hiyo UN imetoa wito kwa pande husika nchini Sudan kukomesha mara moja uhasama na kuwalinda raia, ikieleza kuwa hali ya haki za binadamu nchini humo inazidi kuzorota kwa kiasi kikubwa baada ya wiki mbili za mapigano.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa imevituhumu Vikosi vya Radiamali ya Haraka (RSF) kuwa vinawalazimisha wananchi kuondoka katika makazi yao, na kusema kuwa raia hao wanakabiliwa na uporaji, unyang’anyi na uhaba mkubwa wa chakula, maji, umeme na nishati.

Wakati huo huo, UNHCR imeleeza wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa ghasia baina ya makabila tofauti huko El Geneina, jimbo la Darfur Magharibi.

Katika upande mwingine Kikosi cha Radiamali ya Haraka kimekanusha madai yaliyotolewa ya wale kiliowaita "viongozi wa mapinduzi" waliosema wapigawanaji wa RSF wameshambulia ndege ya Uturuki iliyotumwa Sudan kuhamisha raia waliokwama kwenye vita. RSF imekanusha kuhusika na shambulizi hilo.

Mapema Wizara ya Ulinzi ya ya Uturuki ilikuwa imetangaza kuwa pande zinazohusika na mzozo wa Sudan zimeifyatulia risasi ndege iliyotumwa nchini humo kuhamisha raia waliokwama kwenye vita.

Mamia ya watu wameuawa na maelfu wamejeruhiwa tangu mapigano makali yalipozuka nchini Sudan kati ya vikosi vinavyomtii mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan ambaye pia ni mtawala wa nchi hiyo, na naibu wake, Mohamed Hamdan Dagalo, kamanda wa kikosi chenye nguvu cha msaada wa dharura (RSF). RSF ni kikosi chenye nguvu kilichoundwa na wanamgambo wa Janjaweed ambao kwa miaka mingi walihusika katika mapigano ya mkoa wa magharibi wa Darfur.

Tags