AU yasisitiza haja ya kumalizwa vita na kuanza mazungumzo nchini Sudan
(last modified Sat, 29 Apr 2023 01:51:23 GMT )
Apr 29, 2023 01:51 UTC
  • AU yasisitiza haja ya kumalizwa vita na kuanza mazungumzo nchini Sudan

Umoja wa Afrika AU umesisitizia haja ya kumalizwa mzozo nchini Sudan na kuanza tena mazungumzo kati ya pande hizo mbili zinazozozana.

Kwa mujibu wa televisheni ya Rusia al Yaum, Moussa Faki, Mkuu wa Kamisheni ya AU amesema kuwa, Umoja wa Afrika umezitaka pande mbili zinazohusika na mgogoro wa hivi sasa nchini Sudan kuacha mara moja kushambuliana kijeshi na kuanza tena mazungumzo ya kutafuta suluhu na amani ya kuduumu na kushirikiana na washirika mbalimbali ili kumaliza kabisa vita nchini Sudan.

Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku 3 nchini Sudan kati ya jeshi na vikosi vya radiamala ya haraka yalifikiwa Jumanne iliyopita, lakini hayakuheshimiwa na mapigano yanaendelea hata baada ya pande mbili kukubaliana kurefusha mapatano hayo kwa siku tatu zaidi. 

Majenerali wa kijeshi Sudan, Dagalo na Burhan, marafiki wa jana, mahasimu wa leo

 

Mapigano ya silaha ya kuwania madaraka nchini Sudan yalianza asubuhi ya Jumamosi, Aprili 15 kati ya jeshi chini ya amri ya "Abdel Fattah Burhan" na vikosi vya radiamali ya haraka chini ya amri ya "Mohammed Hamdan Dagalo" maarufu kwa jina la "Hamidati."

Mashambulio ya jeshi la Sudan na vikosi vya radiamali ya haraka yameshasababisha uharibifu mkubwa wa mali ya umma na shida katika usambazaji wa maji na umeme katika baadhi ya maeneo ya Khartoum. Juhudi za kuzileta pande hizo mbili kwenye meza ya mazungumzo bado hayajazaa matunda yaliyotarajiwa.

Wakati huo huo, nchi nyingi na mashirika ya kimataifa yameondoa wafanyakazi na raia wao huko Sudan.

Hadi inaripotiwa habari hii, watu 512 walikuwa wameshauawa na maelfu kujeruhiwa katika mapigano hayo.

Tags