Umoja wa Mataifa waonya kuhusu kuzuka vita vya pande zote nchini Sudan
Umoja wa Mataifa umeonya juu ya hatari ya kuzuka vita vya upande zote na vya muda mrefu nchini Sudan na athari zake mbaya kwenye mipaka ya nchi hiyo.
Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa imeeleza wasiwasi wa taasisi hiyo kuhusu uwezekano wa kutokea vita vya muda mrefu na vya pande zote nchini Sudan, na kusema nchi hiyo inapakana na nchi saba ambazo zote zimekumbwa na migogoro au machafuko ya ndani katika muongo uliopita.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, vita vya sasa vinatokea katika eneo ambalo hali ya ukosefu wa usalama na utulivu wa kisiasa imeongezeka, na hali ya binadamu inazidi kuwa mbaya.
Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imesema, baada ya kuondolewa madarakani Omar Hassan al-Bashir, mwezi Aprili 2019, machafuko yaliyovuruga kipindi cha mpito kulekea utawala wa kiraia yameendelea hadi sasa, na serikali ya kiraia iliyoanzishwa baadaye mwaka huo kupitia makubaliano ya kugawana madaraka, iliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 2021; tangu wakati huo Sudan imebaki bila serikali ya kiraia.
Ripoti ya UN imeendelea kusema: Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa tangu Aprili 15 na kutokana na ongezeko la mapigano kati ya makundi ya kijeshi, ana wasiwasi kuhusu kuibuka vita vya pande zote na vya muda mrefu nchini Sudan, kwa kuzingatia nafasi ya kikanda ya nchi hiyo barani Afrika.
Guterres anaamini kuwa, vita vya kuwania madaraka nchini Sudan sio tu kwamba vinahatarisha mustakbali wa nchi hiyo, bali pia ni cheche inayoweza kulipua moto wa vita nje ya mipaka ya Sudan na kusababisha matatizo na mateso ya miaka mingi. Vilevile anasema vita hivyo yumkini vikachelewesha maendeleo ya eneo hilo kwa miongo kadhaa.
Hadi sasa mamia ya watu wameuawa na maelfu ya wengine wamelazimika kukimbia makazi yao kutokana na vita vinavyoongozwa na majenerali hasimu wa leo na washirika wa jana wa jeshi la Sudan.