Mgogoro wa kisiasa nchini Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9727-mgogoro_wa_kisiasa_nchini_kenya
Wabunge wanane wa Kenya ambao walituhumiwa kwa kutoa matamshi ya uchochezi dhidi ya usalama wa taifa wameachiliwa huru kwa masharti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 22, 2016 03:19 UTC
  • Mgogoro wa kisiasa nchini Kenya

Wabunge wanane wa Kenya ambao walituhumiwa kwa kutoa matamshi ya uchochezi dhidi ya usalama wa taifa wameachiliwa huru kwa masharti.

Muungano wa vyama vya upinzani CORD ulisema kuwa wabunge hao wanane walipaswa kuachiwa kama sharti la kufanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya. Wabunge hao wanane wa mrengo unaotawala Jubilee na ule wa upinzani CORD walikamatwa na kutupwa korokoroni wakituhumiwa kutoa matamshi ya uchochezi ili kuwashawishi wafuasi wao kuanzisha ghasia na machafuko nchini. Hii ni katika hali ambayo wananchi na serikali ya Kenya hivi sasa wanajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika nchini mwakani. Rais Uhuru Kenyatta ambaye tarehe 16 mwezi huu alirejea nchini akitokea ziarani Ubelgiji amekubali kufanya mazungumzo na wapinzani ili kujadili hali ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii ya nchi hiyo. Akizungumza akiwa Ubelgiji Rais Kenyatta alisisitiza kuwa hataruhusu hali ya usalama ya Kenya kwa mara nyingine tena iwe kama ile iliyoshuhudiwa mwaka 2007 na 2008.

Ghasia za uchaguzi zilizosababishwa na ushindani wa wagombea wawili kutoka makabila mawili hasimu huko Kenya ziliitumbukiza Kenya katika machafuko makubwa katika kipindi cha mwezi Disemba mwaka 2007 hadi Januari mwaka 2008; machafuko ambayo yalisababisha mauaji ya watu wengi.

Hitilafu zilizoibuka sasa pia kati ya muungano wa CORD na serikali ya Kenya kuhusu muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo (IEBC) zimezua mgogoro mwingine wa kisiasa nchini humo. Tume hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa chombo hicho ndicho kitakachosimamia uchaguzi mkuu ujao. Hitilafu hizo hadi sasa zimesababisha vifo vya watu wawili na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia mapigano yaliyojiri kati ya wafuasi wa CORD na vikosi vya usalama katika mji wa Kisumu. Aidha watu wengine watatu waliuliwa katika mji wa Siaya huko Kenya.

Muungano wa CORD tangu mwezi Aprili mwaka huu ulianzisha harakati zake za kutaka kufanyiwa marekebisho tume ya IEBC ambayo inapasa kusimamia uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwakani. Raila Odinga Waziri Mkuu wa zamani katika serikali ya umoja wa kitaifa ya Kenya ambayo iliasisiwa baada ya kutokea mgogoro wa baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo, amekaribisha uamuzi wa Rais Kenyatta kufanya mazungumzo. Hali hiyo imepelekea wapinzani kuakhira maandamano ambayo wamekuwa wakiyafanya kila siku ya Jumatatu.

Pamoja na hayo yote, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imeatangaza kuwa ni kinyume cha sheria kufanya maandamano na mikutano ya hadhara nchini ili kuepuka machafuko na kuharibiwa mali za umma. Naye Raila Odinga ambaye alishindwa na Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa mwaka 2013 anasisitiza kuwa tume ya IEBC inapasa kuvunjwa na kufanyiwa marekebisho.

Hii ni katika hali ambayo Rais Kenyatta tayari amewasilisha pendekezo jipya kwa wapinzani. Pendekezo hilo linaeleza kuwa, tume ya wabunge itakayochaguliwa inapasa kuwa na watu 11 kutoka kila upande wa serikali na upinzani. Rais wa Kenya anasisitiza kuwa, wapinzani wanapasa kutekeleza shughuli zao kwa mujibu wa katiba ya nchi. Amesema, kamwe hatoruhusu Kenya iliyo na jamii ya watu milioni 40 kwa mara nyingine tena itumbukie kwenye dimbwi la machafuko. Pamoja na hayo weledi wa mambo wanaamini kuwa katiba ya nchi haipaswi kuzuia uhuru wa kujieleza wa wanaharakati wa kisiasa. Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa mgogoro wa kisiasa wa Kenya unaonekana kupungua kufuatia kuachiwa huru kwa masharti wabunge wanane wa upinzani na serikali na uwezekano mkubwa wa kufanyika mazungumzo ya pande mbili hivi karibuni.