17 wauawa katika mapigano baina ya al-Shabaab na jeshi la Somalia
Kwa akali watu 17 wameuawa baada ya wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab kushambulia kambi ya jeshi katika mji wa Masagawa, katikati ya Somalia.
Mashuhuda wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, watu wasiopungua 17 wameuawa baada ya genge la al-Shabaab kuvamia kambi ya wanajeshi wa Somalia katika mji wa Masagawa, yapata kilomita 300 kaskazini mwa Mogadishu, mji mkuu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Hussein Nur, mmoja wa wakazi wa mji huo amenukuliwa na Reuters akisema kuwa, "Nimeshuhudia maiti 17 zikiwemo za washambuliaji (wanachama wa al-Shabaab) na za walioshambuliwa."
Naye Kapteni Abdullahi Mohamed, mmoja maafisa wa kijeshi katika mji wa Masagawa amethibitisha habari za kutokea shambulizi hilo, na kusema kuwa wanachama 12 wa al-Shabaab wameangamizwa kwenye hujuma hiyo.
Jeshi la Taifa la Somalia limesema katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa Twitter kuwa limezima shambulizi la al-Shabaab na kwamba limeua wanachama wengi wa kundi hilo. Hata hivyo halijasema idadi ya wanajeshi waliouawa.
Haya yanajiri siku chache baada ya magaidi wa al-Shabaab kuvamia kituo cha askari wa kulinda amani wa Uganda katika mji wa Bulamarer, umbali wa kilomita 130 kusini magharibi mwa Mogadishu.
Ingawaje Uganda, Umoja wa Afrika na Somalia hazijasema chochote kuhusu idadi ya wahanga wa shambulio hilo la Ijumaa, lakini genge la kigaidi la al-Shabaab limedai kuwa liliua wanajeshi zaidi ya 137 kwenye hujuma hiyo.