Iran na Sudan kufufua uhusiano wao wa kidiplomasia karibuni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amekutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Sudan kwa mara ya kwanza baada ya miaka saba, ambapo wamekubaliana kufufua uhusiano wa kidiplomasia wa nchio mbili hizi karibuni hivi.
Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mwenzake wa Sudan, Ali Al-Sadiq, walikutana mjini Baku nchini Azerbaijan jana Alkhamisi, pambizoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM).
Wawili hao wamejadiliana kuhusu kufufua uhusiano wa kidiplomasia wa nchi mbili hizi, ambao ulikatika mwaka 2016. Kadhalika wamesisitizia haja ya kuimarishwa uhusiano wa kiasia na kiuchumi wa Tehran na Khartoum.
Amir-Abdollahian amesema, "Pambizoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), ujumbe wetu umekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan na tukajadiliana juu ya kuhuisha uhusiano wa kidiplomasia wa Tehran na Khartoum."
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza kuwa, katika mkutano wake na Ali Al-Sadiq pia wamegusia kuhusu kutatua mivutano iliyopo baina ya nchi mbili hizi, sanjari na njia za kuboresha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi wa pande mbili.
Ikumbukwe kuwa, Sudan ilikata uhusiano wake na Iran mwaka 2016 ikifuata mkumbo wa Saudi Arabia; baada ya Tehran na Riyadh kuhitalifiana kufuatia kuuawa mwanachuoni mashuhuri wa Kishia nchini Saudia, Sheikh Nimr Baqir al-Nimr.
Mwezi uliopita wa Juni, ubalozi wa Iran huko Riyadh ulifunguliwa tena kufuatia makubaliano ya Machi 10 mwaka huu 2023 kati ya Iran na Saudi Arabia huko Beijing chini ya upatanishi wa China. Katika mapatano hayo, nchi hizi mbili zilikubali kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia baada ya kukatwa kwa miaka saba.