Amir Abdollahian: Afrika ni bara lenye fursa nyingi zinazoendelea kuibuka
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema bara la Afrika lililo na jamii kubwa ya vijana, watu wazuri na wenye uchangamfu lina fursa nzuri na zinazoendelea kuimarika kwa manufaa ya wenyeji wa bara hilo na wawawekezaji wa kigeni.
Hossein Amirabdollahian, ambaye anaandamana na Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika safari yake ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika, ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Kuwepo masoko ya aina mbalimbali ya mauzo ya nje na uagizaji bidhaa kutoka nje unahesabiwa kuwa uwanja muhimu kwa ajili ya ushirikiano wa Iran na nchi za Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amesema kuwa nchi za Afrika zina msimamo madhubuti katika kudumisha uhuru wao wa kisiasa. Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akiwa anaongoza ujumbe wa ngazi za juu wa nchi yake na katika kuitikia mwaliko wa Rais William Ruto wa Kenya, amewasili Nairobi, mji mkuu wa Kenya leo Jumatano, kikiwa ni kituo cha kwanza cha safari yake ya kuzitembelea nchi za Kenya, Uganda na Zimbabwe katika bara la Afrika ambapo amelakiwa rasmi na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amesema katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Rais Ruto kwamba Iran na Kenya zina uwezo na nyanja nyingi za ushirikiano, jambo ambalo iwapo litatumiwa vizuri linaweza kusaidia pakubwa katika kuboresha maisha ya watu wa nchi mbili.
Baada ya Kenya, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameelekea Uganda ambapo amelakiwa rasmi na Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo.