Yemen yayatwanga tena kwa makombora maeneo kadhaa ya Israel + Video
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetangaza kuwa, mapema leo Jumanne kumesikika sauti za miripuko mikubwa mjini Tel Aviv na kwenye maeneo mengine ya katikati mwa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.
Vyombo hivyo vya habari vya Israel vimeongeza kuwa, sauti hizo nzito zimetokana na mashambulizi mapya ya makombora yaliyovurumishwa kutokea Yemen.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, sauti za kufyatuliwa makombora ya mifumo ya ulinzi ya miji ya Tel Aviv, Yafa, Rishon Lezion, Ashdodi, Ramat Gan, Elled, Ramleh, Herzliya na Rahofot zimesikika kila sehemu.
Jeshi la utawala wa Kizayuni ambalo linachuja mno habari za vipigo linavyopata kutoka Kambi ya Muqawama, limekiri kufanyika shambulio hilo na kulia ving'ora vya hatari mjini Tel Aviv.
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimetangaza kuwa, karibu walowezi milioni 2 wa Kizayuni wamekimbilia kwenye mashimo na kujificha kwa kuhofia maisha yao na kwamba kwa uchache Wazayuni 20 wamejeruhiwa wakati walipokuwa wamepagawa na kukimbilia kwenye mahandaki kwa hofu na woga mkubwa.
Taarifa nyingine zinasema kuwa, uwanja wa ndege wa Ben Gurion wa mjini Tel Aviv umefungwa na hakuna ndege zinazoingia na kutoka kufuatia mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi ya jeshi la Yemen.
Mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi yamekuja siku chache baada ya Jeshi la Yemen kutangaza kuwa limefanikiwa kuzuia shambulio la pamoja la Marekani na Uingereza kwa kuiangusha ndege ya kivita ya kisasa ya Marekani aina ya F-18 na kulazimisha ndege za maadui kuondoka katika anga ya Yemen.
Msemaji wa jeshi la Yemen Brigedia Jenerali Yahya Saree aliyasema hayo katika taarifa yake juzi Jumapili, baada ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) kusema kuwa ndege yake ya kivita ilidunguliwa kwenye Bahari Nyekundu katika kile ilichodai kuwa ni shambulio la kimakosa lililofanywa na vikosi vyake.