Kumbukumbu ya kuuliwa shahidi Qassem Soleimani
Shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimanim aliuawa tarehe 3 Januari 2020 kwa ndege ya kivita ya jeshi la kigaidi la Marekani akiwa safarini nchini Iraq kwa mwaliko rasmi wa waziri mkuu wa nchji hiyo. ****
Dunia ina anga iliyojaa nyota zinazong'aa nyakati za usiku. Ni mwezi pekee unaotawala anga yake unapoandama hadi unakuwa mwezi kamili. Wakati wa mchana, jua huangaza dunia kwa mwanga na joto lake lisilokoma. Jua, daima linatekeleza wajibu wake, kama ambavyo nguvu za kheri na shari zinavyopigana wakati wote. Katika kila kona ya dunia hii wako maadui wanaowakilisha giza, waliojizatiti kuangamiza kweli na haki. Sawa kabisa na usiku wenye giza totoro, daima hunyemelea mchana kwa makucha yake makali. Nyakati za usiku tunapokuwa tumelala, wako majemedari ambao huwa macho kwa ajili ya kupambana na mashetani waovu wanaotishia wanadamu na ubinadamu.
Usiku wa Ijumaa tarehe 3 Januari 2020, nilikuwa nimelala kwa amani, nikiwazia kwamba ulimwengu ungeendelea kama ulivyokuwa. Lakini ulimwengu haukwenda kwa mujibu wa mawazo yangu. Usiku huo, nikiwa nimelala, ulimwengu ulikuwa umebadilika. Kamanda Qassem Soleimani alisabilia maisha yake katika njia ya kulinda Uislamu na kutetea mataifa yanayodhulumiwa. Niliposikia habari ya kuuawa kwake shahidi, sikuamini, mafisi walikuwa wamemrarua rarua Kamanda wetu na kumkata vipande vipande. Mikono ilikatwa, mguu wake uliangukia upande mmoja, mwili wake ulichomwa moto... Mikono ya Jenerali ilikuwa umekatwa, lakini hakudondosha chini bendera ya Iran na Uislamu. Mwili wake ulikatwa vipande vipande, lakini hakuruhusu ardhi za nchi za Kiislamu zipasuliwe vipande vipande.
Kamanda Soleimani alipigania sio tu Iran bali kwa ajili ya usalama wa eneo zima la Asia Magharibi na mataifa yanayodhulumiwa. Alipambana ili mafisi wa zama hizi wasimtenganishe mtoto na mikono ya mama yake na kisha kumchoma akiwa hai katika moto wa chuki zao. Alifanya hivyo ili wanawake wasiuzwe sokoni kama watumwa. Alipigana ili vichwa vya wanaume visikatwe. Alikuwa ameona jinsi Daesh nchini Iraq, wakisaidiwa na mabwana zao wa Magharibi na washirika wao wa Mashariki, walivyowakata vichwa vijana wapatao 1,200 wasio na hatia, ambao walikuwa wamekamilisha mafunzo katika chuo kikuu cha maafisa wa jeshi na kutupa miili yao mtoni. Wapiganaji wa Daesh walipokezana kuwanajisi kwa zamu zaidi ya wanawake elfu mbili wa Yazidi, kuanzia wasichana wadogo hadi wanawake na mabanati. Alhaj Soleimani alikuwa ameona kwa macho yake jinsi mtoto mchanga avyochukuliwa kutoka mikononi mwa mama yake kisha akachomwa moto kama mwana-kondoo na kurejeshwa kwa mama yake. Uhalifu huu wote wa kutisha uliisumbua nafsi yake yenye huruma, na hili likamtia hima zaidi ya kupambana na kuwatetea wanaodhulumiwa kwa nguvu zake zote. Haikujalisha kwake, mtu anayedhulumiwa alikuwa wa taifa lipi, anazungumza lugha gani, au hata alikuwa na dini gani. Daima, siku zote na kila mahali alikuwa tayari kuwatetea wanyonge na wanaodhulumiwa. ***

Tangu alipokuwa na umri wa miaka ishirini, Haj Qassem alibeba bendera ya kupigania haki na kamwe hakuweka chini bendera hiyo hadi aliposabilia maisha yake kwa ajili ya Iran, kwa ajili ya Uislamu, na katika kuwatetea wanaodhulumiwa.
Shahidi Soleimani, siku zote alitambua vizuri wajibu wake na kuufanyia kazi. Alikuwa makini katika kutimiza wajibu, alijiona kuwa anawajibika mbele ya wanadamu wenzake, na mara zote alitambua vyema hila na mipango ya adui ya kuvuruga utulivu na kuzusha mgawanyiko kati ya makundi mbalimbali. Sawa kabisa na Amirul Muuminan, Ali (as) alivyowaonya maafisa wa utawala wake kuhusu uzembe, kutowajibika na kukosa umakini, kama inavyosewa katika hotuba ya 34 ya Nahj al-Balaghah. Sifa hizi ndizo zinazomfanya kamanda bora na mujahid wa kipekee, kama Haj Qassem, kuweza kuviongoza vikosi vya Muqawama katika medanu pana ya kuanzia Afghanistan hadi Iraq, Syria, Lebanon na Yemen. ***
Nafsi ya Haj Qassem daima ilikuwa katika harakati ya kutafuta ukamilifu na uchamungu. Kamwe hakukengeuka kutoka kwenye njia iliyo sawa na alikuwa daima mstari wa mbele kuwatetea wanaodhulumiwa, kama askari shupavu wa Uislamu. Hakuzembea hata kidogo katika kutimiza wajibu wake.
Haj Qassem daima alikuwa kwenye uwanja wa vita, si kwa ajili yake mwenyewe, bali kwa ajili ya kupigania haki. Ni kamanda ambaye hakuchoka kupigana na maadui wa Uislamu, na alikuwepo katika kila uwanja ambao ilikuwa lazima kuwapo. Jenerali Soleimani, kama kamanda katika Kikosi cha Quds, alitekeleza wajibu wake kwa umakini mkubwa. Uwezo na haiba kubwa ya kamanda huyo wa Uislamu ulimfanya asifiwe na kuvuliwa kofia hata na maadui wake. Aliweza kuzima njama za maadui katika nyanja mbalimbali za ndani na kieneo kwa na kuruka juu ya ardhi za watu wanaodhulumiwa mithili ya tai.
Mwaka 2019, jarida la Marekani la "Foreign Policy" lilimtambulisha Jenerali Qassem Soleimani kama mtu muhimu zaidi kati ya 10 bora katika nyanja za ulinzi wa usalama duniani, katika ripoti yake ya 10 ya kila mwaka ya wanafikra 100 bora zaidi katika nyanja mbalimbali. Jarida hilo liliashiria onyo la Jenerali Soleimani kwa Donald Trump mnamo Julai 2018 na kumnukuu akisema: "Tuko karibu na wewe, kiasi ambacho huwezi hata kukifikiria, tuko tayari."
Siku moja, mmoja wa magavana wa zamani wa mkoa wa Kerman nchini Iran, alikutana na baba wa Shahidi Soleimani na kumwambia: "Hivi unajua jinsi mtoto wako alivyo masuhuri na jinsi anavyoogopwa?" Baba wa Haj Qassem Soleimani alishangazwa na kauli ya mkuu wa mkoa na kusema: “Mwanangu ni askari wa Uislamu. Wanauogopa Uislamu, sio mwanangu. Haj Qassem alilelewa na kukulia kwenye fikra kama hizo, ni ndiyo maana amesema katika wosia wake kwamba: "Nikifa andikeni juu ya jiwe la kaburi yangu kwamba: "Huyu ni Askari wa Qassem Soleimani". XXX
Katika miaka yote ya mapambano yake, Kamanda Soleimani hakuacha kushikama na misingi na kanuni za maadili na ubinadamu. Alitekeleza misingi na kanuni za kupigania haki, uadilifu na kuwahudumisha watu sio kwenye uwanja wa vita pekee, bali pia katika maisha ya kila siku. Alitokana na watu wa kawaida na kuepuka kila kitu kilichomtenganisha na watu. Wakati wa safari zake, alikataa kutumia gari tofauti na la gharama kubwa na kuwaambia waandaji "mnataka kunivunjia hadhi na heshima?" Hakuwa tayari kwa vyovyote kukumbatia maisha ya anasa na ya raha. Licha ya cheo na hadhi yake ya juu.
Moyo na mwenendo huu unakumbusha sifa zilizotajwa na Imam Ali bin Twalib (AS) katika Nahj al-Balagha. Katika mojawapo ya barua zake, Imam anaonya mmoja wa magavana wake akimtaka aishi kama watu wa tabaka la chini katika jamii. Imam anasema katika barua hiyo: Ama baad! Ewe mwana wa Hunaif! Imenifikia habari kwamba mtu mmoja wa Basra amekualika kwenye karamu na wewe ukakimbilia kwenye karamu hiyo. Umekaribishwa kwenye vyakula vya rangi mbalimbali na sahani zilizojaa vyakula. Sikudhani kwamba ungekubali kuwa mgeni kwenye meza ya watu wanaowatenga maskini na kuwaalika matajiri.... Zingatia tonge ambalo unaling’ata kwa meno yako, wacha tonge ambalo hajui uhalali na uharamu wake, na kula unachojua kuwa kimepatikana kwa njia za halali.... Elewa kwamba Imamu wako ametosheka na nguo mbili kuukuu katika dunia yake, na vipande viwili vya mkate kwa chakula chake.... Hakika nyinyi hamuwezi kufanya hivyo, lakini nisaidieni kwa uchamungu, bidii, usafi na kuwa katika njia sahihi...
Kamanda Soleimani alimfuata imamu na mwalimu wake, Ali (AS) katika tabia, mienendo na matendo yake. Hakuwahi kwenda kwenye maeneo yaliyokombolewa kutoka kwa matakfiri wa Daesh akiwa kwenye magari yenye vioo vya kuzuia risasi na vyeusi, na kila mara alifungua mikono yake kukutana na watu wanaoteseka na kuketi nao uso kwa uso.
Daima alihuzunishwa na kuuliwa shahidi wanajihadi wenzake, na alikuwa akiwakumbuka daima katika dua na maombi yake.
Katika msimu wa baridi wa 2018, alialikwa kupokea nishani ya juu zaidi ya kijeshi! Ilikuwa mara ya kwanza kwa jenerali wa Mapinduzi ya Kiislamu kupokea nishani hiyo. Ilikuwa Nishani ya Dhulfikar! Awali alikuwa amepewa Nishani ya Ushindi mara tatu, lakini Nishani ya Dhulfiqar ilikuwa kitu tofauti.

Baada ya kumtunuku Nishani ya Dhulfiqar, Imamu Ali Khamenei, alimpongeza akisema: Kamanda Soleimani ni mtu wa Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Mungu amempa Bwana Soleimani taufiki ya kuweka maisha yake wazi mbele ya mashambulizi ya adui, katika njia ya Mungu na kwa ajili ya Mungu! Kisha alimuombea dua Mungu ampe malipo mema, maisha ya saada na mwisho wake uwe wa kuuawa shahidi!
Naam, Mwaka mmoja baadaye, Kamanda Qassem Soleimani alipata nishani ya juu zaidi ya Muislamu ya kuuawa shahidi. Alifanikisha ndoto yake hiyo ya muda mrefu kupitia mikono ya katili zaidi, yaani Marekani mtendajinai, ambaye si adui wa taifa la Iran pekee, bali pia ni adui wa wanaodhulumiwa kote duniani.
Haj Qassem Soleimani alikuwa ruwaza na mfano bora wa kuigwa na watu wote, hasa kizazi cha vijana. Kwa kujitolea kwake na uaminifu, alianza njia ambayo inapaswa kuendelezwa nyakati zote; Njia ya kuhudumia taifa, ubinadamu, maadili mema, kuwatetea wanaodhulumiwa, na kulinda dini ya Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema peponi roho yake, na amfufue pamoja na Mtume Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu....