Ni yepi malengo ya mradi wa "Sesame Street" katika nchi za Kiislamu?
https://parstoday.ir/sw/news/event-i121810-ni_yepi_malengo_ya_mradi_wa_sesame_street_katika_nchi_za_kiislamu
Hamjambo na karibuni katika kipindi chetu cha wiki hii cha Makala ya Wiki ambacho kitaangazia malengo ya ya mradi wa "Sesame Street" katika nchi za Kiislamu na Kiarabu...
(last modified 2025-10-15T07:49:50+00:00 )
Jan 23, 2025 16:53 UTC
  • Ni yepi malengo ya mradi wa

Hamjambo na karibuni katika kipindi chetu cha wiki hii cha Makala ya Wiki ambacho kitaangazia malengo ya ya mradi wa "Sesame Street" katika nchi za Kiislamu na Kiarabu...

Tofauti na siku za huko nyuma, Ulimwengu wa Magharibi sasa unaingia katika nchi zinazolengwa kupitia vita laini (soft war) vya kutawala na kudhibiti watu kiutamaduni, kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kupenya na kuingia huko pia kunafanyika kwa kutumia njia maalumu, mbinu, mikakati, na zana tofauti. Vyombo vya habari vina jukumu na nafasi kubwa katika mstari wa mbele wa hujuma hiyo.

Miongoni mwa malengo ya vyombo vya habari ni kuhabarisha, kuelimisha, kukuza fikra, kujenga utamaduni na kuzidisha ufahamu, lakini wakati mwingine, malengo ya kimalezi yanafichwa katika machakato huo mzima. Wataalamu wa mawasiliano wanasema, zama tulizomo ni zama za udhibiti na utawala wa vyombo vya habari katika maisha ya binadamu, na umuhimu wa jambo hilo ni mkubwa sana kiasi kwamba umezingatiwa kikamilifu katika mgawanyo wa hatua za historia ya ustaarabu wa binadamu. Mwandishi mtajika wa Marekani, Alvin Toffler, anagawanya ustaarabu wa binadamu katika awamu tatu: Awamu ya kilimo, awamu ya viwanda, na awamu ya baada ya viwanda au zama za mawasiliano na habari. Katika zama za baada ya viwanda, (post-industrial age) mamlaka na nguvu ziko mikononi mwa wale wanaodhibiti mitandao ya mawasiliano na upashaji habari.

Alvin Toffler

Hapa sasa linajitokeza swala la mtindo wa maisha (life style) wa zama hizi. Neno "mtindo" (style) lina maana ya namna, mbinu, na jinsi ya kujieleza, na maisha (life) lina maana ya kuwa hai, kuishi, kuwepo, na muda wa maisha. Hivyo, mtindo wa maisha (life style) ni mtindo, njia na mbinu inayochaguliwa na kutumiwa na kila mtu katika maisha ya kijamii ambayo huunda na kuelekeza tabia, mienendo na matendo yake. 

Mtindo wa maisha wa kila mtu, kundi na taifa unatokana na tamaduni, mila na desturi za mtu, kundi, na taifa hilo. Tunaweza kusema kuwa, utamaduni unaunda kiini kikuu cha mtindo wa maisha, na mtindo wa maisha unahesabiwa kuwa sehemu ya dhihirisho na kielelezo cha nje cha utamaduni wa mtu. Utamaduni, ambao huathiri miundo ya nyenzo na kiroho na kimaanawi za jamii ya wanadamu, huonekana katika kalibu na sura ya mtindo wa maisha. 

Kuhusu mtindo wa maisha, inatosha kusema kuwa aina, mienendo, mapendeleo, na mielekeo makhsusi ya kila taifa au kundi ina uhusiano wa moja kwa moja na shakhsia na hata utambulisho wao. Na zaidi ni kwamba, mtindo wa maisha huakisi maadili, itikadi, na imani za taifa husika.

Wataalamu wa tabia na mienendo wanaamini kwamba, mojawapo ya mambo muhimu katika kubadilisha mtindo wa maisha wa jamii, hasa jamii za ulimwengu wa tatu, ni kubadilisha vigezo vya kitabia na kimwenendo. Kuingizwa bila kizuizi vigezo vya tabia katika jamii za ulimwengu wa tatu kupitia njia mbalimbali kama vile vyombo vya habari, intaneti, na vikundi vya mitandao ya kijamii ndio sababu kuu zaidi ya kubadilika kwa mienendo na tabia na hatimaye kubadilika maisha ya jamii za sasa.   

life style

Sesame Street ni jina la mfululizo wa vipindi vya televisheni ya Marekani kwa ajili ya watoto. Vipindi hivi viko katika sura ya vichekesho na kutoa elimu na vinatayarishwa kwa harakati mubashara au live action animation. Mfululizo wa vipindi hivi vya Sesame Street ni mojawapo ya katuni za muda mrefu zaidi katika historia, ambazo zinatayarishwa kwa ajilii ya watoto na hata watu wazima tangu 1969. Vipindi hivi vimekuwa maarufu kutokana na filamu zake fupi, ishara za kitamaduni, na vichekesho vyake; na utafiti unaonyesha kuwa, vimesababiisha mabadiliko mengi katika utamaduni wa Kimarekani na katika tabia na mienendo ya watoto na vijana.

Awali, serikali na mashirika ya kibinafsi yalikidhi mahitaji ya kifedha ya mradi huu, lakini baada ya muda, kidhahiri kutokana na mafanikio yaliyopatikana, timu ya watayarishaji wake iliweza kukidhi mahitaji ya mradi wao wenyewe. Miongo kadhaa ya kurushwa hewani mfululizo wa vipindi hivyo katika nchi zaidi ya 140 duniani kote na kupata mamilioni ya watazamaji kuanzia Afghanistan hadi Afrika Kusini, vimekuwa sababu ya serikali ya Marekani kufanya uwekezaji maalumu katika mradi huo. Uwekezaji huo sasa umelenga nchi za Kiislamu na Kiarabu kama Syria, Lebanon na Iraq.

"Ahlan Simsim" ndilo jina la Kiarabu la programu hiyo, ambayo imetayarishwa kwa mujibu wa vigezo vya "Sesame Street" ya Marekani. Pamoja na hayo, Sherrie Westin, mmoja wa wakurugenzi wa mfululizo huo, anadai kwamba "Ahlan Simsim" ni bidhaa "ya ndani" kikamilifu iliyoundwa kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani, na kwamba inalenga kutengeneza vipindi vinavyoakisi jamii ya wanaokusudiwa.

Vipindi vya katuni hiyo vimetengenezwa ili kuvutia hadhira iliyokusudiwa. Wahusika wanazungumza katika lahaja tofauti za Kiarabu kuanzia Syria, Lebanon, Jordan na Iraq; hivyo watoto wa nchi hizo wanaweza kuandamana na wahusika wa filamu hiyo.

"Ahlan Simsim" awali iliweza kupata uwekezaji mkubwa, na Taasisi ya MacArthur na vilevile Taasisi ya Lego, kila moja ilitoa dola milioni 100 kwa mradi huu. Muda wa shughuli za mpango huo umekadiriwa kuanza Julai 2021 hadi Juni 2027, na huko Syria umepangwa kwa ajili ya mikoa yote ukilenga zaidi watu jamii za waliowachache kidini na kikaumu.

Mradi huu hauihusu Syria pekee, bali USAID imeshirikiana na Warsha ya Sesame (Sesame Workshop) ili kuzalisha programu ya Ahlan Simsim kwa ajili ya Iraq. Utawala wa Joe Biden ulitenga dola milioni 20 kwa ajili ya mradi huo, na watayarishaji wake walidai kwamba, vijana wa Iraq hawawezi kupata ajira kutokana na sababu za kiuchumi zilizosababishwa na vita (yaani uvamizi wa Marekani na washirika wake huko Iraq) na kwamba wanakabiliwa hatari ya itikadi kali.

Bajeti hiyo ilipaswa kutumika kuwafunza vijana 480 katika ustadi nyepesi (soft skills), 460 katika utengenezaji wa filamu, na 310 katika stadi za kimsingi na za awali na kuanzisha kampeni ya uhamasishaji katika shule tano kwenye mkoa wa la Kirkuk ili kutoa maarifa kwa vijana wa Iraq. Jambo la kuzingatiwa ni kwamba, Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) linashirikiana na Warsha ya Sesame kuzalisha nakala la Kiiraqi ya "Ahla Sesame" kwa lengo eti la "kukuza ushirikishwaji, maelewano, na kuheshimiana kati ya vikundi vya kidini, kikabila na kimadhehebu."

Shirika hilo linasema kuhusu malengo ya ushirikiano huo kwamba: "Ahlan Simsim" nakala ya Iraq pia itatoa zana kwa wasimamizi na walimu kuelimisha vijana wa Iraq katika uwanja wa utengenezaji wa bidhaa za sauti na kusimulia hadithi.

Huenda wewe msikilizaji pia ukapenda kudadisi na kujua kwamba, je, michango na ukarimu huu wa kifedha uliojikita kwa watoto na barobaro wa nchi za Kiarabu kama vile Iraqi unafanyiika kwa sababu za kibinadamu au kuna lengo jingine nyuma ya pazia?

Kwanza, hebu tuashirie nukta hii kwamba, mfululizo wa vipindi hivi vya televisheni, "Sesame Street", hauwezi kuwa kigezo kwa nchi zote duniani na umekabiliwa na upinzai mkali hata ndani ya Marekani kweyewe. Uchunguzi wa maoni uliofanywa mwaka wa 1996 uligundua kuwa, 95% ya watoto wote wa Marekani walikuwa wametazama programu hiyo kufikia umri wa miaka mitatu. Lakini tangu Mei 1970 wapinzani wake walieleza wasiwasi wao kuhusu ujumbe wa kibaguuzi ulioenezwa wa kipindi hicho, miezi michache tu baada ya kuanza kupeperushwa.

Ukosoaji wa awali ulijikita katika kategoria nne: malengo ya kielimu, jinsi malengo yalivyochaguliwa na kufikiwa, athari zinazowezekana za kuonyeshwa katuni hiyo, na taswira yake kuhusu walio wachache na wanawake. Utafiti muhimu zaidi ambao ulielezea athari mbaya za "Sesame Street" ulifanywa na mwalimu Herbert Spregel na mwanasaikolojia Thomas De Kock. Utafiti huo ulibaini kuwa katuni hiyo inazidisha pengo la elimu kati ya watoto masikini na wa tabaka la kati. Pia alikosolewa kwa kuwasilisha taswira ya wahusika wasio wa kweli na kushindwa kuwafundisha watoto mahusiano ya kijamii na jinsi ya kuwa sehemu ya jamii inayowazunguka.

Wataalamu wa elimu nafsi kama Neil Postman pia amesema kuwa Sesame Street inawafundisha watoto tamaduni duni za pop, inadhoofisha elimu ya Marekani, na kuwaondolea wazazi wajibu wao wa kuwafundisha watoto kusoma.

Neil Postman

Mbali na ukosoaji huu wote, kamati ya wanaharakati wa Kihispania pia ilikitaja kipindi hicho cha televisheni kuwa ni cha "kibaguzi." Kutokana na wakati tunatosheka kutaja ukosoaji wote uliofanyika huko Marekani kuhusu ilamu hii ya katuni. Hata hivyo ni lakizima kueleza hapa kuwa, mnamo mwaka wa 2013, kufuatia kuhalalishwa ndoa za watu wenye jinsia moja katika Jimbo la New York, watu wengi walitia saini ombi la kuwataka watayarishaji wa vipindi vya "Sesame Street" kutengeneza kipindi cha ndoa ya Ernie na Bert, wahusika wa mfululizo huo. Jarida la New Yorker pia lilichapisha picha ya wawili hao kwenye jalada lake, likihusisha uhusiano wa wahusika hawa wawili wa kipindi "Sesame Street" na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Marekani kuhalalisha ndoa za watu wa jinsia moja. Suala hili lilikuwa limekwisha sahaulika hadi yalipochapishwa mahojiano na Mark Salzman, ambayo kwa mara nyingine yaliwakumbusha mamilioni ya mashabiki wa filamu hiyo kwamba Ernie na Bert walikuwa mashoga. Salzman, ambaye alikuwa mwandishi wa mfululizo huo wa filamu za katuni kwa miaka kumi na tano, alisema katika mahojiano na jarida la Curtis, ambalo linahusu masuala ya mashoga, kwamba alipata mwongozo na ilhamu kutokana kwenye uhusiano wake na mshirika wake katika kutayaisha wahusika wawili wakuu wa "Sesame Street", na kwamba Bert na Ernie ni wahusika katika mfululizo hu ni mabaradhuli na wanaojihusisha ya maingiliano ya kingono baina ya watu wenye jinsia moja. Tangazo hilo lilizua utata mwingi, na watetezi wa haki za watoto waliwashutumu vikali watayarishaji wa mfululizo huo.

Kwa hivyo, tunaona kwamba licha ya matangazo yote na gharama kubwa ziazotumiwa kutengeneza mfululizo huo, mtindo wa maisha unaoenezwa na kupigiwa debe na vipindi hivyo vya televisheni ni tofauti na mtindo wa maisha katika nchi za Kiislamu, zikiwemo nchi za Kiarabu. Hapa ndipo tunapoelewa malengo yake na kupata jibu la swali tulilouliza mwanzoni mwa kipindi hiki kuhusu malengo ya gharama za mamilioni ya dola zinazotolewa na serikali ya Marekani na mashirika ya nchi hiyo kwa ajili ya kutayarisha vipindi hivyo. Kueneza utamaduni wa Kimarekani, kufundisha ushoga na kuwatwisha watoto na watu wazima mtindo wa maisha wa Kimarekani...