Jul 21, 2023 03:37 UTC
  • Iran yamuita balozi wa Sweden kulalamikia kuvunjiwa heshima Qurani

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemuita balozi wa Sweden mjini Tehran kulalamikia hatua ya serikali ya nchi hiyo ya Ulaya Magharibi ya kuruhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amemkabidhi balozi huyo wa Sweden mjini Tehran barua rasmi ya malalamiko na kumtaka aiwasilishe kwa serikali ya Stockholm.

Hii ni baada ya jeshi la polisi la nchi hiyo ya Ulaya kumpa idhini kwa mara nyingine tena raia wa Sweden mwenye asili ya Iraq, Salwan Momika kuidhalilisha nakala ya Qur'ani Tukufu mjini Stockholm.

Momika hapo jana aliikanyaga na kuipiga mateke nakala ya Qurani Tukufu nje ya Msikiti mkuu mjini Stockhol, huku akipewa ulinzi na maafisa usalama wa nchi hiyo ya Ulaya.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema katu Jamhuri ya Kiislamu haitoruhusu kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini kwa kisingizio chochote.

Wananchi Waislamu wa Iran wakiitetea na kuiadhimisha Qurani Tukufu

Kan'ani amesema kitendo hicho cha kichochezi na kinachogusa nyoyo na hisia za Waislamu bilioni mbili kote duniani hakipaswi kuhalalishwa kwa kisingizio cha uhuru wa kujieleza.

Ikumbukwe kuwa, 28 Juni ambayo ilisadifiana na sikukuu ya Mfunguo Tatu yaani Idul Adh'ha, Salwan Momika alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu mjini Stockholm akiwa amepewa ulinzi kamili na polisi wa Sweden.

Viongozi mbalimbali wa Iran walitoa matamshi ya kulaani jinai hiyo ya kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Sweden, kuanzia Rais, Spika wa Bunge na Mkuu wa Idara ya Mahakama, hadi Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mpaka Mkuu wa Taasisi ya Utamaduni na Mawasiliano ya Kiislamu.

Tags