Sisitizo la Iran la kutekelezwa makubaliano ya usalama na Iraq
Akizungumza tarehe 11 Septemba hapa mjini Tehran na Bafel Talabani, Mkuu wa Muungano wa Kizalendo wa Kurdistan ya Iraq, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya ametaka makubaliano ya usalama yaliyofikiwa kati ya Iran na Iraq yatekelezwe haraka iwezekanavyo.
Takwa kama hilo pia lilitolewa karibuni na balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Iraq, alipokutana na kuzungumza na Rais pamoja na Waziri Mkuu wa serikali ya utawala wa ndani ya eneo la Kurdistan ya Iraq huko katika mji wa Erbil. Mohammad Kazem Al-Sadegh, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Baghdad, amekutana na kuzungumza na Masrour Barzani, Waziri Mkuu na Rais Nechirvan Barzani katika safari aliyofanya katika Mkoa wa Kurdistan wa Iraq.
Uhusiano wa Kurdistan ya Iraq na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni muhimu sana. Pande hizi mbili zina uhusiano mkubwa na mkongwe wa kiutamaduni. Mbali na ukaribu uliopo baina ya Wakurdi wa Iran na Iraq, sehemu kubwa ya watu na viongozi wa Kurdistan ya Iraq waliishi nchini Iran, na sehemu kubwa ya Wakurdi wa Iran pia wanaishi katika Kurdistan ya Iraq. Ingawa idadi ya Wasuni wa Iraq si ndogo, lakini kimadhehebu jamii za Wasuni na Washia zimekuwa zikiishi pamoja kwa amani na kuheshimiana.
Eneo la Kurdistan daima limekuwa mwenyeji wa umati mkubwa wa waumini wanaoshiriki katika matembezi ya Arbaini ya Imam Hussein (as). Kuhusiana na hilo, Balozi wa Iran mjini Baghdad, Al-Sadegh, akizungumza karibuni katika kikao na serikali ya ndani ya Kurdistan ya Iraq, amepongeza na kuishukuru serikali ya eneo la Erbil kwa kutoa msaada kwa washiriki wa matembezi ya Arbaini ya Imam Hossein (as).
Suala muhimu ni kwamba, ijapokuwa mipaka ya Iran na eneo la Kurdistan haijawahi kushuhudia mzozo baina ya pande mbili, lakini eneo hilo la Iraq daima limekuwa likitumiwa na makundi ya kigaidi na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya maslahi ya taifa hili. Suala hili limekuwa likilalamikiwa mara kwa mara na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo vikosi vya kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimeshambulia mara kadhaa makao makuu ya makundi ya kigaidi na maadui wa mfumo wa Kiislamu wa Iran wanaojificha katika eneo hilo la Iraq.
Kuhusiana na hilo Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao chake na Bafel Talabani amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka Iraq iliyo huru, yenye ustawi na maendeleo na kubainisha kuwa, kuwepo magaidi katika eneo la Kurdistan na operesheni zao dhidi ya usalama wa Iran kunakinzana na katiba ya Iraq inayosisitiza kuwepo uhusiano wa kirafiki na kidugu na majirani zake na kusema kuwa hakuna chama au kundi lolote linaloruhusiwa kudhuru usalama wa majirani wa Iraq.
Kwa upande mwingine, baada ya machafuko ya mwaka jana nchini Iran, wakati magaidi na wakufurishaji walipotumia mipaka ya eneo la Kurdistan ya Iraq kuzusha machafuko na ukosefu wa usalama nchini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilionyesha azma yake thabiti ya kutatua suala la uwepo wa magaidi na waasi katika eneo la Kurdistan ya Iraq. Katika vikao baina ya maafisa wa kisiasa na usalama wa Iran na Iraq, pande mbili zilitia saini makubaliano ya usalama na kuweka makataa ya kuhitimisha uwepo wa magaidi na waasi kaskazini mwa Iraq.
Katika kikao cha karibuni baina ya Hossein Amirabdollahian na mkuu wa Muungano wa Kizalendo wa Kurdistan ya Iraq na pia katika kikao cha balozi wa Iran nchini Iraq na viongozi wa Erbil, ulazima wa kutekelezwa makubaliano hayo ya usalama ulisisitizwa. Kuhusiana na hilo, Nachirvan Barzani, Rais wa Eneo la Kurdistan ya Iraq amesema katika kikao na Al-Sadegh, balozi wa Iran mjini Baghdad kwamba, kwa kuzingatia kuwa Iran ni jirani muhimu wa eneo la Kurdistan, uhusiano na pande mbili hizi ni muhimu sana. Amesisitiza kwamba eneo hilo linaheshimu makubaliano ya usalama kati ya Iraq na Iran na kuwa kamwe halitaruhusu kuibuka katika eneo hilo tishio lolote la usalama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.