Wafungwa wa Iran na Marekani waachiliwa huru
Wafungwa wa Iran na Marekani wameachiliwa huru leo baada ya mataifa haya mawili kutekeleza makubaliano ya kubadiliishana wafungwa.
Ripoti za karibuni kabiisa zinasema kuwa, wafungwa wa Kimarekani waliokuwa wakishikiliiwa hapa nchini baada ya kuachiliwa huru tayari wamesafirishwa kwa ndege maalumu kwenda Doha Qatar.
Awali msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alikuwa amesema kuwa, Wairani watano waliofungwa nchini Marekani wangeachiliwa huru leo, na wafungwa watano wa Marekani wangeachiliwa huru hii leo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Nasser Kan'ani amesema hayo mbele ya waandishi wa habari leo Jumatatu na kuongeza kwa kusema: "Kwa mujibu wa taarifa za karibuni kabisa nilizo nazo, suala la kubadilishana wafungwa lingefanyika leo.
Vile vile amesema kuwa, raia wawili wa Iran walioachiliwa huru nchini Marekani watarejea humu nchini, na raia mwingine mmoja atakwenda nchi nyingine kutokana na familia yake kuweko huko. Raia wengine wawili wa Iran wataendelea kuweko Marekani kutokana na kuishi huko kwa muda mrefu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amefafanua zaidi kwa kusema kuwa, kuna uwezekano wa kufanyika mazungumzo ya upatanishi kuhusu kufutwa vikwazo pambizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.
Kuhusu kuachiliwa fedha za Iran zilizokuwa zinashikiliwa kinyume cha sheria nje ya nchi, Kan'ani amesema: Kulindwa vilivyo haki za taifa la Iran ni jukumu la serikali zote za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Serikali mbalimbali zinazoingia madarakani humu nchini zinatumia mbinu zao za kisiasa za kulinda haki za taifa, na serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendelea kufuatilia kwa dhati suala la kulindwa kikamilifu haki za taifa hili.