Sep 24, 2023 10:54 UTC
  • Iran: Hatutotuma balozi wetu mpaka serikali ya Sweden ichukue hatua nzuri kuhusu Qur'ani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amefanya mazungumzo na waziri mwenzake wa Sweden na kusisitiza kuwa, Tehran haitotuma balozi wake nchi humo hadi pale serikali ya Stockholm itakapochukua hatua nzuri za kuheshimiwa Qur'ani Tukufu nchini Sweden.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Hossein Amir-Abdollahian alionana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Tobias Billström, wakati waziri huyo alipomtembelea Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwenye sehemu aliyofikia mjini New York, Marekani alikokwenda kwa shughuli za kidiplomasia ambapo kwa mara nyingine Tehran imesisitizia wajibu wa kubadilishwa sheria za Sweden ili zisiruhusu kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini hasa ya Waislamu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia mazungumzo kadhaa yaliyofanyika baina yake na waziri huyo wa mambo ya nje wa Sweden kabla ya kuonana ana kwa ana na kusema kuwa, ingawa mazungumzo hayo yalihusu nyuga tofauti, lakini uwanja muhimu zaidi kwa Iran ni kuhakikisha kuwa serikali ya Sweden inapiga marufuku kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na matukufu mengine ya kidini. 

Mkimbizi wa Iraq anayesakwa kwa kutenda jinai, akiivunjia heshima Qur'ani Tukufu kwa ulinzi kamili wa polisi wa Sweden

 

Amezungumzia jinsi Waislamu bilioni 2 duniani wanavyoumizwa na jinai za kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na matukufu yao mengine huko Sweden na nchi nyingine za Ulaya na amemwambia waziwazi waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo ya Ulaya kwamba, haikubaliki kabisa kwa serikali ya Stockholm kuruhusu kuvunjiwa heshima matukufu ya watu bilioni mbili kwa madai ya kulindwa maadili ya Sweden. 

Amesema, kwa mara nyingine tunaitaka serikali ya Sweden itekeleze vizuri majukumu yake ya kuheshimu imani ya Waislamu bilioni mbili duniani. 

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden amesema katika mazungumzo hayo kwamba chuki dhidi ya Uislamu hazina nafasi katika serikali ya nchi yake na kwamba anaunga mkono kuishi pamoja kwa kuvumuliana na kuheshimiana watu wa dini tofauti.