Qalibaf: Mataifa ya Kiislamu yasimamishe mashambulizi ya Wazayuni
(last modified Wed, 08 Nov 2023 03:33:06 GMT )
Nov 08, 2023 03:33 UTC
  • Qalibaf: Mataifa ya Kiislamu yasimamishe mashambulizi ya Wazayuni

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amelaani vikali mashambulizi ya kinyama utawala wa Kizayuni huko Gaza na kusisitiza kuwa, mataifa ya Kiislamu yana wajibu wa kusimamisha dhulma na hujuma hizo za kikatili za Wazayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Muhammad Bagheri Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran alisema hayo jana katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Algeria, Ibrahim Boughali, ambapo wamejadiliana kuhusu matukio yanayoendelea Gaza.

Qalibaf amebainisha kuwa, nchi za Kiislamu zinapasa kuchukua hatua za dharura za kukomesha jinai za kutisha zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na hatia wa Gaza.

Amesema wahanga wakuu wa mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni katika eneo hilo lililozingirwa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu ni watoto wadogo na wanawake.

Spika wa Bunge la Iran ameashiria nafasi ya makundi ya muqawama katika kukabiliana na chokochoko za Wazayuni na kueleza kwa: Nguvu ya harakati ya muqawama imeulazimisha utawala huo kutoa majibu ya woga. 

Amesema utawala wa Kizayuni umegeuka na kuwa chombo cha mauaji kisichodhibitiwa na kilichopindukia kwa kufanya uhalifu kupitia kupuuza na kukiuka sheria zote za kimataifa.

Jinai za kutisha za Israel Ukanda wa Gaza

Qalibaf sanjari na kuashiria ushirikiano wa kibunge wa Iran na Algeria ameeleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kuogoza mkutano wa dharura wa Kamati ya Kudumu ya Palestina ya Jumuiya ya Kimataifa ya Mabunge (IPU) katika ngazi ya Maspika na wakuu wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu kujadili kadhia ya Gaza.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Kitaifa la Algeria, Ibrahim Boughali ameashiria mkutano wa IPU uliofanyika hivi karibuni nchini Angola na kubainisha kuwa: Licha ya kuendelea mauaji ya kimbari na jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina wa Gaza, lakini kikao hicho cha jumuiya ya mabunge hakikuwa na tija yoyote ya maana.

Aidha ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuendelea kusimama, kuwatetea na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina na kuongeza kuwa: Algeria ni nchi ya wapenda uhuru na wanamapinduzi, kwa msingi huo, msimamo wetu wa kuwaunga mkono Wapalestina na kutetea haki zao upo thabiti na imara.

Tags