Kuongezeka uwepo wa wanamaji wa Iran katika Bahari Nyekundu
Meli ya kivita ya Alborz imerudi tena katika Bahari Nyekundu ikiwa ni katika Meli za Kikosi cha 94 cha Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kupitia Lango-Bahari la Bab al-Mandab. Manowari hiyo ya Alborz ilijiunga na Meli za Kusini za Jeshi la Wanamaji Desemba 2019 baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa na kuwekwa humo mifumo mipya ya kiteknolojia.
Mwanzoni mwa 2009, manowari za wanamaji za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilianza harakati zao katika Bahari Nyekundu (Sham) ili kuhakikisha usalama wa njia za meli, kupambana na maharamia baharini na masuala mengine, na kuingia tena manowari ya Alborz katika bahari hiyo kunatathminiwa katika mtazamo huo.
Bahari Nyekundu na lango la Bab al-Mandab zina nafasi na umuhimu mkubwa katika uchumi na biashara ya dunia, na ni kutokana na sababu hiyo, ndipo ikachukuliwa kuwa na umuhimu mkubwa wa kistratijia, ambapo uwepo wa jeshi la majini la Iran katika bahari hiyo una umuhimu maradufu. Aidha kuwepo maharamia katika Bahari Nyekundu kumeongeza pakubwa haja ya kulindwa meli za kibiashara na za mafuta za Iran na mashua za uvuvi. Katika miezi ya hivi karibuni, kuongezeka mivutano katika Bahari Nyekundu na juhudi za Marekani za kuunda muungano wa jeshi la majini dhidi ya Yemen kwa kisingizio cha mashambulizi yake dhidi ya maslahi na meli zinazoelekea Palestina inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni hususan bandari ya Eilat, kumezidisha maradufu umuhimu wa kuwepo Iran katika eneo hilo. Bahari Nyekundu ni mojawapo ya vivuko vikuu vya meli za biashara ya kimataifa, na takriban meli 16,000 za kibiashara na kijeshi na karibu asilimia 30 ya mafuta duniani hupitia eneo hilo kila mwaka. Kwa hivyo, Bahari Nyekundu imekuwa nguzo muhimu sana kiasi cha kugongana maslahi na malengo ya nchi kadhaa za pwani, kikanda na kimataifa kuhusiana na jambo hilo. Bahari hiyo pia ni njia muhimu ya kistratijia kwa harakati za kijeshi za nchi za Magharibi kuelekea eneo la Ghuba ya Uajemi.
Umuhimu wa jeshi la wanamaji kwa usalama wa taifa na mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama nchi yenye pwani ndefu zaidi kwenye mipaka yake ya kaskazini na kusini ni jambo lisilopingika. Isitoshe, kuwepo vilivyo jeshi lake la majini katika maji ya eneo ya Bahari Nyekundu na ya kimataifa kama vile Bahari ya Hindi, Atlantiki na Pasifiki kuna muhimu usiopingika katika uwanja wa kuonyesha nguvu na kudhaminiwa maslahi yake kieneo na kimataifa.
Katika miaka ya hivi karibuni, nafasi ya Jeshi la kistratijia la wanamaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeimarika katika maji ya Ghuba ya Uajemi na kaskazini mwa Bahari ya Hindi na vile vile Bahari Nyekundu baada ya kupata meli na nyambizi mpya zilizotengenezwa humu humu nchini. Ili kutambua uwezo na nguvu za kimkakati za kikosi hicho, ni muhimu sana kuchunguzwa kiwango cha nguvu, yaani uwezo wake wa kuendesha na kudhibiti shughuli na operesheni za majini katika maeneo ya mbali na hasa baharini. Ili kufikia lengo hilo, ni muhimu kwa kikosi hicho kuwa na manowari na meli kubwa za kimkakati ambazo zina uwezo wa kutekeleza operesheni za mbali na za kistratijia zinazokiwezesha kupambana na vitisho vyovyote vile.
Kuhusiana na suala hilo, kutengenezwa manowari ya Makran ni hatua ya kwanza ya kuwepo jeshi la kistratijia la Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika maji ya kimataifa. Kwa kutimia jambo hilo, ndoto ya muda mrefu ya jeshi la wanamaji katika uwanja wa kutekeleza operesheni muhimu za baharini kwa kiwango cha kimataifa imetimia, ambapo hatua ya kwanza katika uwanja huo ilichukuliwa Mei 2021 baada ya kutumwa msafara wa kundi la manowari zilizoongozwa na meli ya kivita ya Makran kutoka Bandari ya Makran hadi kwenye Bahari ya Atlantiki. Baada ya miaka mingi ya juhudi za kuboresha uwepo wa jeshi la kistratijia la majini la Iran baharini, hatua madhubuti zimechukuliwa katika uwanja huo, na miundo mbinu na meli zinazofaa zimeandaliwa katika uwanja huo. Hivi sasa makamanda wa kistratijia wa jeshi la wanamaji la jeshi hilo, wanaandaa uwanja wa kufanikisha suala hilo sambamba na stratijia kubwa ya kitaifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa hakika jeshi la wanamaji ni mhimili muhimu wa utawala wa Iran katika bahari na ni nguvu ya kistratejia inayoathiri nyanja za jumla na za kistratijia za nchi. Na hasa tukizingatia kuwa hatua za kikosi hicho zinaathiri moja kwa moja mwenendo wa sera muhimu za kitaifa.