Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuitembelea Misri karibuni
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian anataziwa kuitembelea Misri ndani ya siku chache zijazo, huku utawala wa Kizayuni ukiingiwa na kiwewe kutokana na kuendelea kuimarika uhusiano wa Tehran na Cairo.
Shirika la habari la IRNA leo Jumatatu limenukuu tovuti ya habari ya Arabi 21 iliyoripoti kuwa, ziara ya mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran mjini Cairo inatazamiwa kuimarisha uhusiano wa pande mbili wa Jamhuri ya Kiislamu na Misri.
Kwa mujibu wa tovuti ya Arabi 21, jitihada hizi za kuhuisha uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Misri zinakuja wakati huu ambao ni hasasi na nyeti katika eneo la Asia Magharibi.
Wakati huo huo, gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeeleza kuhusu wasi wasi ilionao Tel Aviv kutokana na kuendelea kuimarika uhusiano na ushirikiano baina ya Cairo na Tehran, wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni unaendeleza mashambulizi ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Disemba, afisa mmoja wa ngazi za juu wa Misri alisema nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na Iran zinatazamiwa kufufua kikamilifu uhusiano wa pande mbili wa kidiplomasia, na hata kubadilishana mabalozi.
Rakha Ahmad Hassan, mwanachama wa Baraza la Masuala ya Kigeni la Misri alisema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik la lugha ya Kiarabu na kueleza kuwa, "Kubadilishana mabalozi ni suala ambalo yumkini litafanyika karibu hivi."
Ikumbukwe kuwa, Misri na Iran zilikata uhusiano wao mwaka 1980 baada ya nchi hiyo ya Kiarabu kumpokea mtawala aliyepinduliwa wa Iran, Mohammed Reza Pahlavi; mbali na Cairo kuutambua utawala wa kibaguzi wa Israel.