Iran yawanyonga magaidi wanne maajenti wa Mossad
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i107764-iran_yawanyonga_magaidi_wanne_maajenti_wa_mossad
Idara ya Mahakama ya Iran imewanyonga watu wanne waliopatikana na hatia ya kufanya kazi na shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel, Mossad, na kupanga njama ya shambulio la bomu dhidi ya kiwanda cha Wizara ya Ulinzi katika mkoa wa Isfahan katikati mwa Iran.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 29, 2024 09:16 UTC
  • Iran yawanyonga magaidi wanne maajenti wa Mossad

Idara ya Mahakama ya Iran imewanyonga watu wanne waliopatikana na hatia ya kufanya kazi na shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel, Mossad, na kupanga njama ya shambulio la bomu dhidi ya kiwanda cha Wizara ya Ulinzi katika mkoa wa Isfahan katikati mwa Iran.

Shirika la habari la Mizan, lenye uhusiano na Idara ya Mahakama ya Iran, limeripoti leo Jumatatu kwamba wafungwa hao wanne, waliotambuliwa kwa majina ya Mohammad Faramarzi, Mohsen Mazloum, Vafa Azarbar na Pejman Fatehi, waliingia Iran kinyume cha sheria kutoka eneo lenye mamlaka ya ndani la Kurdistan nchini Iraq.

Taarifa hiyo imesema, mnamo Julai 23, 2022, walikuwa wakipanga kutekeleza operesheni ya kulipua jengo katika kiwanda kimoja cha mji wa Najafabad, ambacho huunda zana za kijeshi na vipuri vya makombora kwa ajili ya Wizara ya Ulinzi.

 Hata hivyo, walitambuliwa na kukamatwa mara moja na askakri usalama wa  Iran siku chache kabla ya kutekeleza hujuma ya kigaidi.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa wanne hao wamepatikana na hatia ya ushirikiano wa kijasusi na Israel na walihukumiwa kifo na Mahakama ya Mapinduzi ya Kiislamu mnamo Septemba 18, 2023.

Gazeti la Mizan limeeleza kuwa magaidi hao walikuwa wamesajiliwa na mwanachama mashuhuri wa kundi la kigaidi la Komala lililo dhidi ya Iran na linalopigania kujitenga, lenye makao yake makuu katika eneo la Kurdistan la Iraq. Wanne hao walijiunga na shirika la ujasusi la Israel, Mossad, karibu mwaka mmoja na nusu kabla ya operesheni yao ya kigaidi nchini Iran.

Walikuwa wamepitia mafunzo katika kambi za kijeshi za Mossad katika nchi kadhaa za Afrika na hata walifanya mikutano na Mkurugenzi wa Mossad, David Barnea.

Mnamo tarehe 29 Disemba mwaka jana pia magaidi waliokuwa wakishirikiana na Mossad walinyongwa katika mkoa wa kaskazini magharibi mwa Iran wa Azarbaijan Magharibi baada ya kukutwa na hatia ya kupanga njama dhidi ya usalama wa nchi.