Amir Abdollahian: Iran na Pakistan zimekubaliana kupanua ushirikiano wa kupambana na ugaidi
(last modified Tue, 30 Jan 2024 11:09:05 GMT )
Jan 30, 2024 11:09 UTC
  • Amir Abdollahian: Iran na Pakistan zimekubaliana kupanua ushirikiano wa kupambana na ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Tehran na Islamabad zimekubaliana kupanua ushirikiano kwa ajili ya kupambana na ugaidi.

Hossein Amir Abdollahian jana alifanya ziara nchini Pakistan ambapo alikutana na kuzungumza na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje, Kamanda wa Jeshi na Waziri Mkuu wa nchi hiyo. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwaambia waandishi wa habari  kabla ya kuondoka Islamabad kwamba amefanya mazungumzo muhimu na viongozi wa ngazi ya juu wa Pakistan katika ziara yake nchini humo. Amesema, katika mazungumzo hayo, pande mbili za Tehran na Islamabad zimekubaliana kuendeleza kwa kasi zaidi ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za kiuchumi, kibiashara, utalii, nishati na katika sekta nyingine.  

Amir Abdollahian ameongeza kuwa: Serikali za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan zimeafikiana kwamba kwa mujibu wa jedwali lililoainishwa vivuko vitano vipya vya mpakani viongezwe kati ya nchi mbili hizi jirani.  

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa   mipaka salama ya nchi hizo mbili inapaswa kuwa mipaka ya kukuza biashara, uchumi na utalii kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan zinaamini kuwa, mipaka ya nchi mbili si mahali pa ugaidi na hujuma za kigaidi. 

Baada ya operesheni ya Iran ya kupambana na ugaidi dhidi ya ngome za magaidi huko Pakistan na shambulizi la Pakistan dhidi ya maeneo kadhaa ya mpakani nchini Iran, ambayo kwa mujibu wa Islamabad yalikuwa maficho ya magaidi wa Pakistan; kumekuwapo uvumi juu ya sintofahamu katika  uhusiano wa muda mrefu wa nchi hizi mbili muhimu za Kiislamu, lakini viongozi wa  Tehran na Islamabad kwa upande wao wamesisitiza udharura wa kuzuia mivutano baina yao.