Iran yalaani vikwazo vya upande mmoja vya Magharibi dhidi ya mataifa huru
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika makao makuu ya Umoja wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva amesema: Vikwazo vya upande mmoja vimepelekea kukithiri machafuko ya kibinadamu kote duniani.
Ali Bahrain, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi amesema katika mkutano wenye anuani "Athari za hatua za upande mmoja kwa utumaji misaada ya kibinadamu na utendaji wa watendaji wa kibinadamu" kwamba, uharamu wa vikwazo vya upande mmoja umethibitishwa kikamilifu leo. Na imedhihirika wazi kwamba, athari za uharibifu wa vikwazo hivi zimezidisha migogoro ya kibinadamu na ukiukwaji wa haki za kimsingi za binadamu.
Marekani inahesabiwa kuwa nchi inayoongoza kwa uwekaji vikwazo duniani, ikiwa na rekodi kubwa zaidi ya kutumia kila aina ya vikwazo dhidi ya nchi zingine kwa ajili ya kufanikisha malengo na maslahi yake.
Wakati huo huo, gazeti la Marekani la New York Times limeandika katika ripoti kwamba baadhi ya nchi za Magharibi zinazounga mkono vikwazo dhidi ya Russia zimeongeza uagizaji wa bidhaa na hasa nishati kutoka nchi hiyo tangu Februari mwaka huu.
Nchi za kambi ya Magharibi ambazo zimeongeza kwa kiasi kikubwa ununuzi wa bidhaa kutoka Russia, zimeshiriki kikamilifu katika kupinga operesheni za kijeshi za Moscow nchini Ukraine, zikiwemo nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na zile zinazounga mkono vikwazo dhidi ya Russia.