Apr 29, 2024 11:40 UTC
  • Kamanda wa IRGC: Iran mdhamini wa usalama wa Ghuba ya Uajemi

Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema mkakati wa Iran ni kuendeleza amani, usalama na udugu katika Ghuba ya Uajemi na Mlango Bahari wa Hormuz.

Admirali Alireza Tangsiri ameyasema hayo katika mahojiano siku ya Jumatatu kwa mnasaba wa Siku ya Kitaifa ya Ghuba ya Uajemi.

Ameongeza kuwa siku hii ya kitaifa ni kumbukumbu ya kumalizika miaka 117 ya kukalia kwa mabavu Ureno eneo la Ghuba ya Uajemi.

Akiashiria umuhimu wa kistratijia wa eneo hilo la bahari, Tangsiri amesema maji ya kina kirefu zaidi kwenye pwani ya Ghuba ya Uajemi na njia bora za maji ziko upande wa Iran.

Kanda hiyo ni "muhimu sana" linapokuja suala la usalama, amebainisha, akisisitiza kwamba Iran inasisitiza kuwasilisha ujumbe wake wa amani na urafiki kwa nchi zote za kikanda. Iran inataka kuweka usalama kamili katika Mlango-Bahari wa Hormuz na imezihakikishia usalama meli 83 zinazopita kwenye mkondo huu wa maji kila siku.

Kamanda wa IRGC, hata hivyo, amesisitiza kuwa wageni wanaovuruga usalama wa Ghuba ya Uajemi na Mlango wa bahari wa Hormuz hawataruhusiwa kuendelea kufanya hivyo.

Ghuba ya Uajemi ni muhimu kwa Iran, ambayo ina urefu wa pwani wa kilomita 1,375, amebainisha. Ameongeza kuwa Ghuba ya Uajemi ina nafasi muhimu kiuchumi, kwani asilimia 40 ya gesi ya dunia na asilimia 62 ya mafuta unapatikana katika eneo hili. Siku ya leo ya tarehe 10 Ordibehesht kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani inafahamika nchini kuwa Siku ya Taifa ya Ghuba ya Uajemi.

Siku hii imetengewa jina hilo kutokana na baadhi ya pande zenye chuki dhidi ya Iran, kufanya njama za kutaka kupotosha historia, kwa kulipa eneo hilo majina mengine yasiyo na msingi. Jina la kihistoria la Ghuba ya Uajemi limetafsiriwa katika lugha mbalimbali kwa jina hilo hilo au kwa jina la Bahari ya Pars. Inafaa kuashiria hapa kuwa, Ghuba ya Uajemi ni ya tatu kwa ukubwa duniani baada ya Ghuba ya Mexico na Ghuba ya Hudson.