May 01, 2024 07:18 UTC
  • Iran na Uganda kuimarisha ushirikiano katika sekta ya kilimo

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Viwanda na Madini ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inatilia maanani ushirikiano wa kilimo na Uganda katika uga wa kilimo nje ya mipaka ya nchi, mafunzo na ushirikiano wa wataalamu na watafiti.

Ezatollah Akbari Talar Poshti, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Viwanda na Madini ya Bunge la Iran ameyasema hayo katika kikao chake na Rukia Isanga Nakadama, Naibu Waziri Mkuu wa Uganda aliyeko safarini mjini Tehran. Ameongeza kuwa, uhusiano na maingiliano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uganda umekuwa katika kiwango kizuri tangu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini, na mashauriano ya ngazi ya juu ya kisiasa ya viongozi wa nchi hizo mbili yamepitia mchakato mzuri.

Akbari Talar Poshti amekumbushia safari ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi nchini Uganda mwaka jana na kusema, Iran inatilia mkazo umuhimu wa uhusiano na nchi za Kiafrika na inataraji kuwa ziara za viongozi wa Iran na Uganda zitaboresha kiwango cha uhusiano na kuharakisha ushirikiano katika nyanja tofauti.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu wa Uganda, ambaye ameshiriki katika Maonyesho ya Uwezo wa Kuuza Nje Bidhaa za Iran (Iran Expo 2024), amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nchi ya Kiislamu yenye nguvu kubwa katika eneo la Magharibi mwa Asia, na Uganda inafanya jitihada za kuimarisha uhusiano na Iran. 

Rukia Isanga Nakadama amesema Uganda na Iran zinaweza kushirikiana katika nyanja mbalimbali za kuwawezesha wanawake zikiwemo sekta za sayansi na teknolojia, afya na kazi za mikono.

Tags