May 01, 2024 10:53 UTC
  • Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu: Ghaza ndilo suala la kwanza kwa Ulimwengu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Ghaza ndilo suala la kwanza kwa Ulimwengu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ameyasema hayo leo asubuhi alipohutubia hadhara ya maelfu ya walimu na wanautamaduni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Allamah Morteza Motahari na Siku ya Mwalimu, na akaeleza kwamba, leo Ghaza ndilo suala kuu kwa ulimwengu; na Wazayuni na waungaji mkono wao wa Marekani na Ulaya hawawezi kuliondoa suala la Ghaza kwenye ajenda ya fikra na maoni ya umma ya walimwengu.
 
Ayatullah Khamenei amesema, mwenendo wa Marekani katika kadhia ya Ghaza ni uthibitisho kwamba Washington haiwezi kuaminika na akaongezea kwa kusema, "tazameni vyuo vikuu vya Marekani na Ulaya, inapasa mashinikizo dhidi ya utawala wa Kizayuni yazidi kuongezwa siku hadi siku".
 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha pia kwa kusema "angalieni vipi Wamarekani na vyombo vyenye uhusiano na wao wanavyoamiliana na upinzani wa maneno tu dhidi ya Israel; wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani hawajafanya uharibifu, hawajatoa kaulimbiu za kufanya uharibifu, hawajaua mtu, hawajachoma moto mahali popote na wala hawajavunja kioo, lakini hivi ndivyo wanavyotendewa".
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu akihutubia hadhara ya walimu na wanautamaduni

Ayatullah Khamenei ameongezea kwa kusema: "mwenendo huu wa Wamarekani umeonyesha usahihi wa msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kutoiangalia Marekani kwa jicho zuri, ambao kwa hakika ni kutilia nguvu kaulimbiu yenu mnayotoa ya 'Mauti kwa Marekani' na umemuonyesha pia kila mtu kwamba Marekani ni mshirika katika uhalifu". 

 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua kwa kusema, "kile ambacho mtu anakiona katika matendo, ni kuwa bega kwa bega na kushirikiana Marekani na utawala wa Kizayuni katika jinai hii kubwa na katika dhambi hii isiyosameheka katika Ukanda wa Ghaza. Wao wanashirikiana katika uhalifu. Mtu anawezaje kuutazama kwa jicho zuri mfumo kama huu na utawala kama huu? Inawezekanaje? Au awe na imani na maneno yake!"

Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba Palestina ni ya "wamiliki wake wa asili" na hatua zozote za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni hazitatuliza hali ya mambo katika eneo la Asia Magharibi.

Amefafanua kwa kusema: "Palestina lazima irudi kwa wamiliki wake wa asili. Palestina ni ya watu wa Palestina, wakiwemo Waislamu, Wakristo na Wayahudi; Palestina ni yao wao na inapasa irejee kwao wao... hivi ndivyo tatizo la eneo la Asia Magharibi litakavyotatuliwa".

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, "baadhi wanadhani kuzilazimisha nchi jirani zianzishe uhusiano na utawala wa Kizayuni kutaondoa tatizo. Hapana, wamekosea”.../