May 02, 2024 11:14 UTC
  • Maoni ya Kiongozi Muadhamu: Gaza ndilo suala la kwanza kwa Ulimwengu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Gaza ndilo suala la kwanza kwa mfumo wa Ulimwengu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, aliyasema hayo Jumatano asubuhi jijini Tehran alipohutubia hadhara ya maelfu ya walimu na wanautamaduni kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Allamah Morteza Motahhari na Siku ya Mwalimu nchini.

Miezi 7 imepita tangu kuanza mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Jinai ambazo Wazayuni wamezitenda dhidi ya watu wa Gaza, mauaji ya kimbari na uharibifu uliotokea ni mambo ambayo yamepelekea suala la Gaza kujulikana na wengi duniani.

Mwamko wa walimwengu dhidi ya jinai za Wazayuni sasa umongezeka na wakati huo huo propaganda za uongo za Wazayuni na vyombo vya habari vya Magharibi zimezidi kudhihirika na kutotiliwa maanani tena.

Kuhusiana na hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesema: "Leo suala la Gaza ni suala la kwanza la dunia, yaani katika ngazi ya kimataifa... "tazameni vyuo vikuu vya Marekani, Australia na katika nchi tofauti za Ulaya. Kuna mwamako wa mataifa kuhusu Gaza na sasa suala hili ni la kwanza duniani.

Suala jingine ni kwamba, mazingatio ya umma wa dunia kuhusu kadhia ya Gaza ni makubwa kiasi kwamba Wazayuni na waungaji mkono wao hususan Marekani hawawezi tena kusimamisha maandamano makubwa ya wananchi katika ngazi ya kimataifa, hata wafanye nini. Kwa hakika kushindwa kwao kuzuia maandamano hayo kunaashiria pigo kubwa walilopata.

Kiongozi Muadhamu amesema: "Wazayuni na waungaji mkono wao wa Marekani na Ulaya wanafanya kila wawezalo kuliondoa suala la Gaza katika ajenda ya maoni ya umma duniani lakini hawatafanikiwa."

Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Columbia Marekani katika maandamano ya kuunga mkono wanaoandamana kulani jinai za Israel dhidi ya Gaza na uungaji mkono wa Marekani kwa jinai hizo.

Nukta ya tatu ni kuwa sasa ulimwengu umefahamu ni kwa nini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiuarifisha utawala wa Kizayuni wa Israel kama utawala unaotenda jinai na Marekani kuwa muungaji mkono mkuu wa jinai za utawala huo wa Kizayuni.

Wananchi wa Iran katika kipindi cha miaka 45 iliyopita daima wamekuwa wakipiga nara za "Mauti Kwa Marekani" na "Mauti kwa Israel." Wapinzani na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakikosoa na kulaani nara na msimamo huo wa mfumo wa Kiislamu na wananchi wa Iran.

Leo jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza na uungaji mkono wa Marekani kwa mauaji hayo ya kimbari ni mambo ambayo yamethibitisha usahihi wa msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Khamenei pia amesema kuhusiana na hilo: "Leo dunia nzima inaona mwenendo wa utawala wa Kizayuni; watu zaidi ya elfu thelathini wameuawa katika kipindi cha miezi sita, ambapo kwa uchache nusu yao ni wanawake na watoto; hili si jambo dogo, ni ukatili mkubwa, ni ukosefu wa huruma. Si jambo dogo kwamba mbwa huyu kichaa anaua watoto wa Kipalestina, wazee na wanawake. Hili ni moja ya nukta zinazothibitisha usahihi wa msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa watu wa dunia.  Katika kipindi cha miaka 45 sasa watu wa Iran wamekuwa wakipiga nara ya 'Mauti kwa Utawala wa Kizayuni wa Isarel.' Hivi sasa msimamo huu wa haki wa Jamhuri ya Kiislamu umeweza kuthibitika kuwa ni sahihi."

Suala jingine muhimu ni kwamba maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya  Marekani na ukatili wa polisi dhidi ya wanafunzi hao ni jambo ambalo limeibua maswali kuhusu usahihi wa madai ya Marekani ya eti kuwa ni mtetezi wa haki za binadamu. Sasa ni wazi kwamba madai ya Marekani kuhusu haki za binadamu hutumika tu kwa ajili ya kukandamiza, kubana na kutoa mashinikizo dhidi ya nchi nyingine na kama kisingizio cha kuingilia mambo ya ndani ya nchi hizo.

Kuhusiana na nukta hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema "angalieni ni vipi Wamarekani na vyombo vyenye uhusiano nao wanavyoamiliana na upinzani dhidi ya Israel. Wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani hawajafanya uharibifu, hawajatoa kaulimbiu za kufanya uharibifu, hawajaua mtu, hawajachoma moto mahala popote na wala hawajavunja kioo, lakini hivi ndivyo wanavyotendewa."

Hatua ya utawala wa Marekani ya kukandamiza wanafunzi wanaounga mkono Palestina na kupinga Israel pia inaonyesha usahihi wa msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu wa kutoiamini Marekani na kwamba kwa hakika Marekani ni mshirika mkuu katika jinai za Israel dhidi ya Wapalestina..

Yamkini watawala wa Marekani wakadai kuwa wana huruma na kadhalika lakini ni uongo mtupu na ni kinyume na ukweli. Anachokiona mwanadamu kivitendo ni namna Marekani inavyoshirikiana kwa karibu na utawala ghasibu wa Israel katika utekelezaji wa jinai za kutisha na zisizosameheka za utawala huo dhidi ya Wapalestina wasio na hatia, hasa wanawake na watoto.